Waziri Maige ajitosa kwenye madini

Na Joachim Mushi

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, amejitosa kwenye mgogoro wa uchimbaji madini hapa nchini huku akiapa kupambana na kampuni ya African Barrick Gold, ambayo ni mwekezaji mkubwa kuliko wote hapa Tanzania.

Katika hali ya kutatanisha, Maige ametaka Serikali kuipokonya kampuni ya Barrick leseni ya madini kwenye wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, na badala yake ipewe kikundi kimoja kilichopo kwenye jimbo lake la Msalala.

Kampuni ya Mkumi Exploration iliyosaini mkataba na Barrick ni mmiliki halali wa leseni ya kutafuta madini (prospecting licence) kwenye eneo la Jomu, Mwazimba, wilayani Kahama iliyokabidhiwa na Wizara ya Nishati na Madini baada ya kushinda tenda mwaka 2011.

Barrick, ambayo imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 2 kwenye migodi mbali mbali hapa nchini, inalalamika kuwa eneo lake hilo limevamiwa na kikundi cha Kasi Mpya Gold Mining Corporative Society (KAGAMICO) ambacho kinaungwa mkono na Maige.

Kikundi cha KAGAMICO kimekuwa kikichimba dhahabu kwenye eneo hilo tangu mwaka 2009 kinyume na sheria licha ya kuwa Barrick ndiyo mmiliki halali wa leseni ya eneo hilo.

“Mimi nitafanya kazi yangu ya kuwatetea na mimi niseme niko tayari kulipa gharama yoyote itakayoendana na kusema ukweli kwenye jambo hili,” Maige aliwaambia wanachama wa kikundi cha KAGAMICO katika mkutano nao hivi karibuni wilayani Kahama.

Katika mkutano huo, Maige alitoa shutuma kali kwa Barrick waziwazi kufuatia mgogoro huo wa uchimbaji wa madini, huku akiishutumu kampuni hiyo kuwa haiitakii mema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
“Kwa haya yanayotokea sasa, mimi nasema Barrick haiipendi CCM … Wana zaidi ya leseni 200 maeneo mbalimbali. Nilikuwa kwenye kamati ya Bomani ya kupitia maeneo hayo. Hakuna kampuni ambayo ina leseni nyingi kama kampuni hii,” alisema Maige huku akiitaka Barrick iachie eneo la Mwazimba kwa wachimbaji wadogo.

Hata hivyo, wadau wa sekta ya madini wamekosoa kauli ya Maige kwa kusema kuwa kampuni ya Tanzanian Royalty Exploration Corporation, inayomilikiwa na raia wa Canada, Jim Sinclair, ndiyo inaongoza kwa kuwa na leseni nyingi za madini Tanzania.

Aliitaka serikali ya kijiji Mwazimba kufanya kila jitihada kukisaidia kikundi cha KAGAMICO dhidi ya Barrick ambayo ina leseni halali ya eneo hilo.

“Mkiwafananisha hawa (KAGAMICO) na wale (Barrick) hawawezi, kwa hiyo watazameni (KAGAMICO) ni wenzenu wanaganga njaa,” alisema waziri huyo.

“Ukiwashindanisha hawa na Barrick, wanasema Barrick anatoa nyingi hawa hawatoi nyingi, utawauwa,” Maige alimwambia mwenyekiti wa serikali ya kijiji Mwazimba.

Maige alisema kuwa Barrick tayari wanachimba dhahabu ya kutosha Bulyanhulu na kuwataka waliachie eneo la Mwazimba kwa wachimbaji wadogo.

“Lile chepe moja tu lile la Barrick pale Bulyanhulu kama lile alilopewa zawadi Rais mstaafu wakati fulani, lile tu linatosha kabisa kulisha jimbo letu kwa mwaka mzimam,” alisema.

“Kale katofali kamoja tu kakidondoka kale, jimbo zima la Msalala hakuna njaa.”

Rais mstaafu Benjamin Mkapa anadaiwa kupokea zawadi ya dhahabu kutoka kwa mgodi wa Geita unaomilikiwa na kampuni ya AngloGold Ashanti wakati alipoenda kuuzindua mgodi huo uliopo mkoani Mwanza mwaka 2000.

Maige alimwandikia barua Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, tarehe 8 Februari, 2011, kumtaka waziri huyo mwenzake kusitisha mpango wa kuwahamisha wachimbaji wadogo kwenye eneo hilo la Barrick.

“Endapo kwa vyovyote vile itashindikana kupatiwa eneo hilo la Mwazimba, basi watengewe eneo lao na wapatiwe kabla ya kuondolewa mahali walipo sasa,” anasema Maige kwenye barua hiyo yenye kumbukumbu DMNRT/288/401/01/58.
 
Maige alimtaka Ngeleja kuhakikisha kuwa katika kipindi cha mpito wakati serikali inashuhulikia mgogoro kwenye eneo hilo, serikali iwaachie wachimbaji wadogo waendelee na shuhuli zao kwenye eneo hilo la Barrick.

Akitekeleza maombi ya Maige, Ngeleja alimwamuru Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja Bahati Matala, kusimamisha zoezi la kuwahamisha wachimbaji wadogo kwenye eneo linalomilikiwa kisheria na kampuni ya Barrick.
 
“Ili kutoa nafasi ya kulishughulikia suala hili kikamilifu, nakuagiza usitishe zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika eneo husika hadi hapo tutakapokamilisha uchunguzi wa malalamiko yaliyoletwa kwetu,” alisema Ngeleja kwenye barua yake kwa DC wa Kahama.
 
Katika barua hiyo ya tarehe 17 Februari 2011 yenye kumbukumbu namba DA.170/264/01, Ngeleja alipeleka nakala kwa Waziri Mkuu, Maige na kikundi cha KAGAMICO bila kuwapa nakala Mkumi Exploration ambayo ni mhusika mkuu kwenye mgogoro huo.
 
Kampuni tanzu ya Barrick, Mkumi Exploration Limited, ilipewa leseni ya eneo hilo na Wizara ya Nishati na Madini kwa kutumia utaratibu wa tenda mwaka 2010 chini ya sheria mpya ya madini.

Kikundi cha KAGAMICO, ambacho hakikuwa miongoni mwa kampuni zilizo omba tenda hiyo, kinadai kuwa kilipeleka maombi kwa ajili ya leseni ya uchimbaji mdogo (primary mining licence) katika eneo hilo tangu mwaka 2009.
 
Hata hivyo ilibainika kuwa leseni waliyopewa KAGAMICO ni kwa ajili ya uchimbaji katika eneo tofauti na Mwazimba ambalo kampuni ya Barrick ndiyo yenye leseni halali. 

Vipimo (coordinates) vya leseni ya uchimbaji mdogo ambayo kikundi cha KAGAMICO imepewa na Wizara ya Nishati vinaonesha kuwa wamepewa eneo jingine nje ya eneo la Barrick ambalo wachimbaji hao wadogo wamekuwa wakiendelea kuchimba kunyume na sheria tangu mwaka 2009.
 
“Kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa Mbunge wa Msalala, Mheshimiwa Maige, kwenda kwa Mkuu wa Wilaya wa Kahama kwa njia mbali mbali ikiwepo ujumbe mfupi wa simu (SMS),” alisema afisa mmoja wa serikali mkoani Shinyanga.

Imedaiwa kuwa katika mmoja ya mawasiliano hayo ya njia ya simu, Waziri Maige alimtuhumu mkuu wa wilaya kuwa “kibaraka” wa Barrick.
 
Baadhi ya maafisa wa serikali wameshangazwa na Ngeleja kuingilia kati sakata hilo ni kinyume cha sheria kwani Kamishna wa Madini ndiyo mwenye mamlaka ya kutoa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
 
“Pamoja na kuwa Ngeleja ni waziri mwenye dhamana, sheria mpya ya madini inampa Kamishna wa Madini mamlaka wa utoaji wa leseni. Waziri anahusika na migodi tu, si utoaji wa leseni za utafutaji au uchimbaji mdogo wa madini,” alisema mwanasheria mmoja wa serikali.
 
Nayo kampuni ya Barrick imeonesha kusikitishwa kwake na kitendo cha serikali kushindwa kuwazuia wachimbaji wadogo kuvamia eneo lake wakati kampuni hiyo ikiwa ni mmiliki halali wa leseni.
 
Barrick wamesema kuwa tayari wameshatumia zaidi ya dola za Marekani milioni 3 (sawa na sh. bilioni 4.5) kwenye eneo la Jomu lenye ukubwa wa kilomita za mraba zaidi ya 49.
 
“Ni jambo ambalo linakatisha tamaa sana. Tumefuata taratibu zote za kisheria lakini bado haki zetu kama wamiliki halali wa leseni iliyotolewa na Kamishna wa Madini kwenye eneo la Jomu inaporwa,” alisema Teweli Teweli, meneja mawasiliano wa Barrick.

“Barrick inatambua haja ya kusaidia wachimbaji wadogo wadogo kumiliki kisheria maeneo ya uchimbaji. Lakini ni muhimu sana kwa sheria na taratibu husika zikafuatwa.”

Waziri Ezekiel Maige