WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Selina Kombani ameipongeza taasisi ya Seed Trust kwa jitihada zake za kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake na watu wenyeulemavu. Bi. Kombani ametoa pongezi hizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tasisi ya Seed Trust, Magreth Mkanga (MB), leo jijini Morogoro alipokuwa akifungua kongamano la kujadili namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watuwenye ulemavu.
Alisema Bi. Mkanga (MB) kupitia taasisi yake na nje ya hapo amekuwa mstari wa mbele kapaza sauti juu ya haki za watu wenyeulemavu na vitendo vya ukatili kwa ujumla.
“…Binafsi napenda kumpongeza sana Mama Mkanga kwa kweli yeye amekuwa mstari wa mbele katika utetezi wa haki za walemavu…namuona kule bungeni tuko naye na mara zote anapaza sauti juu ya haki za kundi hili…,” alisema Bi. Kombani.
Aidha alimtaka kila mwana jamii kushiriki katika kupaza sauti juu ya kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watu wenye ulemavu kwa ujumla. Alisema vitendo vya ukatili vimekuwa vikiathiri jamii yote bila kujali matabaka hivyo kutaka nguvu ya kila mmoja ishiriki katika kuvipinga kwa hali na mali vitendo hivyo.
Hata hivyo alivitaka vyombo vya sheria yaani mahakimu nchini kuweka kipaumbele kwenye kesi za vitendo vya kikatili kwa makundi yote ili kuhakikisha wahusika wanaovunja sheria wanapambana na mkono wa sheria kwa wakati kupunguza vitendo hivyo.
Kongamano hilo la siku mbili lililoandaliwa na taasisi ya Seed Trust kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) limeshirikisha wadau mbalimbali, taasisi na idara ambazo shughuli zao zinagusa na kuhusika kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Miongoni mwa wadau walioshirikishwa katika kongamano hilo ni pamoja na Jeshi la Polisi kupitia madawati ya jinsia baadhi ya mikoa, Idara ya Mahakama, Idara ya Ustawi wa Jamii, wanasheria na baadhi ya wawakilishi toka asasi za kiraia nchini.
Kwa upande wake, Bi. Mkanga (MB) alimshukuru Waziri Kombani na Serikali kwa ujumla kwa kuonesha ushirikiano kwa taasisi yake na kuongeza kuwa kitendo hicho kinaonesha jitihada za Serikali kukabiliana na vitendo vya kikatili kwa wanawake na walemavu kwa ujumla.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com