Waziri Kigoda Ashangazwa na Mvinyo wa Nyanya

Mvinyo wenye kileo unaotengezwa na nyanya.

Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko Dk. Abdalah Kigoda akipata maelezo kuhusu mvinyo wenye kileo unaotengezwa na nyanya.

WAZIRI wa Viwanda Biashara na Masoko Dk. Abdalah Kigoda ameshangazwa na mvinyo wenye kileo unaotengezwa na tunda la nyanya. Kigoda alishangazwa na hali hiyo hivi karibuni alipokuwa akikagua mabanda ya maonesho ya SIDO ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika mkoani Mbeya.
Dk. Kigoda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maonesho hayo alitembelea banda la mradi wa Muunganisho Vijijini (MUVI) na kijionea mvinyo huo unasadikiwa kuwa ni wa kwanza kutengezwa nchini Tanzania kwa kutumia tunda la nyanya.
Kigoda aliyekuwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abasi Kandoro pamoja na Mkurugenzi wa SIDO Taifa, Bw. Maiko Laizer, alijikuta akitumia muda mrefu ndani ya banda hilo tofauti na mabanda mengine aliyotembelea.
Akiwa katika banda hilo, waziri aliweza kuuliza maswali kadhaa ili kujiridhisha juu ya mvinyo huo. Kigoda, alishangazwa zaidi pale alipoambiwa kuwa, kwa mara ya kwanza tunda la nyanya limeweza kutengeneza mvinyo wenye kileo nchini Tanzania kupitia mradi wa MUVI mkoani Iringa. Mvinyo huo una kilevi cha asilimia 12%
Akielezea mvinyo huo, Ofisa Masoko wa Mradi wa MUVI, Frederick Mumbuli, alisema mradi wa MUVI katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ongezeko la thamani katika kile ambacho wakulima wanazalisha, wamebuni njia mbadala ili kuleta tija zaidi, hii ikiwa ni hatua mojawapo.
“Mradi wa MUVI unafanya kazi katika dhana ya mnyororo wa ongezeko la thamani hivyo unaangalia zao tangu likiwa shambani hadi kumfikia mlaji wa mwisho, mradi ulibaini kuwa zao la nyanya lilikuwa likiharibika kutokana na kukosa soko, lakini sasa napenda kuwahakikishia wakulima wa nyanya na watanzania kwa ujumla kuwa nyanya inaweza kubadilisha mwenendo wa soko kupitia mvinyo huu,” alisema Mumbuli.
“Nyanya tenga moja huuzwa kati ya sh. 5,000 na 10,000 bei ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kumgandamiza mkulima, lakini tenga moja linaweza kutengeneza chupa za mvinyo zipatazo 100, ambapo chupa moja huuzwa kati ya sh. 4500 na 5000 kwa mahesabu ya haraka haraka jumla ya mauzo ni sh. 500,000”
Mumbuli alizidi kufafanua na kusema, Ukitoa gharama za usindikaji pamoja na vifungashio faida ni kati ya sh. 200,000 na 250,000 kwa tenga hivyo unaweza kuona namna tenga moja linavyoweza kutengeneza faida.
Naye mwenyekiti wa kikundi cha wasindikaji wa mvinyo huo kiitwacho, Imalutwa Food Processors, bwana Fredrick Mgwabi na Bi, Rosemery Mtavangu kutoka Tanangozi Food Processors kwa pamoja wamesema kuwa tunda la nyanya sasa linaweza kuwa na faida tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Katika hatua nyingine, Bi. Mtavangu alisema tayari wafanyabiashara wakubwa wameanza kujitokeza na kutoa oda ya bidhaa hiyo.
Katika maonesho hayo chupa za mvinyo huo zipatazo 120 ziliuzwa huku baadhi ya wakaaza wa mji wa Mbeya waliobahatika kuonja mvinyo huo wakionesha uhitaji mkubwa.
Mradi wa MUVI ambao upo chini ya wizara ya viwanda na biashara na hapa mkoani unasimamiwa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO.