Na Beatrice Lyimo, MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amewataka Viongozi wa Serikali mkoani Kagera kuhakikisha wanasimamia matumizi sahihi ya vifaa vya misaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea hivi karibuni mkoani humo.
Waziri Jenista aliyasema hayo leo wakati alipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kukagua taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo shule za msingi ileega na nyamilima ambazo zimeathirika kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi.
Katika ziara hiyo, Waziri Jenista alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kyerwa kuhakikisha ukarabati wa taasisi za umma unakamilika kwa wakati ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii.
Aidha Waziri Mhagama amewataka wananchi kwa umoja wao kushirikiana katika kurejesha hali ya makazi kutokana na idadi kubwa ya wanaohitaji msaada huo.
“Nitoe rai kwa wananchi wote kwa umoja wenu kushirikiana kwa hali na mali katika kuhakikisha mnarejesha hali yenu ya makazi kutokana na idadi kubwa ya wanaohitaji msaada huo”, alisema.
Mbali na hayo Waziri Jenista aliwataka wanafunzi walioathirika na maafa hayo kutokatisha masomo bali waendelee kama ratiba ya vipindi inavyoonyesha.
Kwa upande wake mwalimu kutoka shule ya Msingi Ileega Anna Mollel ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kusaidia familia zilizopatwa na athari ya tetemeko hilo na kuzipa kipaumbele shule, nyumba za walimu pamoja na taasisi nyingine za Serikali.