Waziri Haroun awasilisha bajeti ya Wizara ya Baraza la Wawakilishi

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman amewasilisha katika Baraza la Wawakilishi, Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, huku wizara hiyo ikijivunia mafanikio lukuki.
Waziri Haroun katika hotuba yake hiyo anataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kupanuliwa kwa wigo wa kuwawezesha wananchi kiuchumi, utekelezaji wa malengo ya idara ya mikopo, kuboreshwa kwa sekta ya ushirika, kuimarishwa kwa kamisheni ya kazi, uboreshaji wa malengo ya idara ya ajira na utekelezaji wa malengo ya idara ya usalama na afya kazini.
Kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi, Waziri Haroun alisema katika kipindi cha mwaka 2011/2012 jumla ya wajasiriamali 94 (Unguja 64 na Pemba 30) wamepatiwa mafunzo juu ya usimamizi wa biashara, uwekaji wa kumbukumbu, utafutaji masoko, uandaaji wa mpango wa biashara na uanzishaji wa mtandao wa biashara ili kutanua soko.
“Mafunzo hayo yalisaidia kuwajengea uwezo na ari wajasiariamali na hata baadhi yao kuhamasika kushiriki katika mashindano ya Mama Shujaa wa Chakula wa Tanzania na wengine katika maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi, kwa gharama zao wenyewe.”
Mafanikio mengine kwa mujibu wa Waziri Haroun ni kuanzishwa kwa Soko la Jumapili kwa wajasiriamali wazalishaji wadogo wadogo ili waweze kuuza bidhaa zao.Hatua hiyo imetokana na kilio cha muda mrefu kuhusiana na kukosa eneo la kufanyia biashara zao.
Fursa hiyo sasa imewezesha wajasiriamali wasiopungua 60 kupeleka bidhaa zao katika soko hilo lililopo Mwembekisonge Michenzani kila Jumapili, hatua iliyowawezesha wajasiriamali hao kupata fursa ya kutanua soko la bidhaa zao kutokana na kupata oda nyingi.
Kwa upande wa mikopo, katika mwaka uliopita wa fedha, Idara ya Mikopo chini ya Wizara hiyo imetoa mikopo 195 yenye thamani ya Sh milioni 143.5 kupitia Mfuko wa Kujitegemea wa Unguja na Pemba.
Waziri Haroun alisema Idara hiyo pia imeendelea kuratibu shughuli za Mfuko wa JK/AK (Jakaya Kikwete/ Amani Karume) ambao unasimamiwa na Benki ya Watu wa Zanzibar.Kupitia Mfuko huo, jumla ya Sh bilioni 1.529 zilikuwa zimetolewa hadi kufikia mwezi Mei 2011.
Kuhusu ushirika katika mwaka wa fedha uliopita, Wizara hiyo imeweza kuwawezesha vijana 3,854 kuanzisha miradi miradi ya kiuchumi kupitia vyama vya ushirika kwenye wilaya zote za Unguja na Pemba, ambapo moja ya manufaa ya mpango huo ni kusajiliwa kwa vikundi 327 vya ushirika ambavyo kwa sehemu kubwa vinaundwa na vijana.
Kwa upande wa ajira katika mwaka ujao wa fedha, Wizara hiyo kwa mujibu wa Waziri Haroun, imekusudia kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na uwekaji wa taarifa za soko la ajira, kuzalisha ajira 2,000 kupitia sekta mbalimbali za umma na binafsi.