WAZIRI wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ameipongeza Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa kuandaa mpango maalumu wa kutoa mikopo kwa wastaafu wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF ikiwa ni fursa itakayowainua kiuchumi wastaafu hao.
Waziri Kabaka ametoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizinduwa rasmi mpango wa mikopo kwa wastaafu wa Mfuko wa Penseni wa LAPF, mpango utakaowawezesha wastaafu sasa kuchukua mikopo na kuendelea kukidhi maitaji yao kipindi hicho. Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Waziri Kabaka alisema Benki ya Posta na Mfuko wa Penseni wa LAPF hauna budi kupongezwa kwa hatua ya kulikumbuka kundi la wastaafu ambalo kimikopo lilikuwa limesahaulika.
“…Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Benki ya Posta Tanzania pamoja na Mfuko wa Pensheni wa LAPF kwa kubuni mpango huu maalum wa kuwasaidia wastaafu kimaisha na kuwawezesha kumudu gharama za mahitaji yao na kukabiliana na ukosefu wa muda mfupi wa fedha wanazohitaji kwa kuwapatia mikopo,” alisema Waziri Kabaka.
Aliongeza kuwa mpango huo utawasaidia wastaafu kipindi cha maisha yao mapya ya kustaafu kwani licha ya muda huo wengi kuwa na kipato kidogo cha mapato lakini gharama za maisha kwao hazipungui na badala yake huendelea kupanda, jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwao.
“…Ninafarijika kuona kwamba Benki ya Posta pamoja na LAPF mmeliona hili na kulifanyia kazi, na hatimaye kuja na huduma hii ya mikopo. Lengo mahususi la mpango huu ambao kwa kiasi fulani umeanza kutekelezwa ni kuwapa faraja na kuwasaidia wastaafu katika kukidhi mahitaji yao mbalimbali, ili kuweza kuboresha maisha yao na maslahi kwa ujumla,” alisema waziri huyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi akizungumza katika hafla hiyo, alisema mkopo huo ni wa kwanza na wa aina yake katika soko la mabenki nchini hivyo wanaamini utatoa hauweni kwa wastaafu wa LAPF.
Akifafanua zaidi alisema mstaafu anayehitaji kuwa na dhamana huku riba inayotozwa kwa mkopo huo kuwa ni ndogo yaani asilimia 12 tu kwa mwaka ukilinganisha na mikopo mingine. “…Mkopo huu umewekewa bima, hivyo endapo mkopaji atafariki familia yake haitaendelea kudaiwa. Hivyo wastaafu wote wa mfuko wa LAPF wanaweza kupata mikopo hii ambayo marejesho yake ni kati ya mwaka mmoja hadi miaka mitatu,” alisema Moshingi.
Alisema huduma za mikopo hiyo ni za haraka na bora na zitatolewa kwa matawi yote ya Benki ya Posta Tanzania hivyo kuwataka wahitaji wote wastaafu wa Mfuko wa Penseni wa LAPF kwenda katika matawi hayo popote nchini kupata maelezo ya nini cha kufanya kabla ya kupata mkopo huo.
Hata hivyo TPB kwa kushirikiana na LAPF wamezishauri taasisi za fedha nyingine zikiwemo Benki kuangalia namna ya kuweka mipango ya kusaidia wastaafu nchini kwani kundi hilo lina kiasi kikubwa cha fedha ambacho kikitumiwa vyema kinaweza kuleta mchango mkubwa katika uchumi wan chi ya Tanzania. Hafla hiyo pia iliyohudhuriwa na viongozi waandamizi na wafanyakazi wa TPB na Mfumo wa Penseni wa LAPF ilishirikisha pia baadhi ya wastaafu ambao baadhi walieleza wameanza kunufaika na mpango huo wa mikopo kwa wastaafu.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com