Na Joachim Mushi
ALIYEKUWA Waziri wa Fedha nchini Tanzania, Dk. William Mgimwa aliyefariki dunia nchini Afrika Kusini anatarajiwa kuzikwa Tanzania Januari 6, 2014. Mwili wa kiongozi huyo wa Taifa unatarajia kuwasili nchini Tanzania Januari 4, 2014 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.
Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera na Uratibu Bunge, William Lukuvi alisema tayari ratiba ya mazishi ya marehemu Dk. Mgimwa imeandaliwa na kamati ya mazishi taifa na ile ya Mkoa wa Iringa anaotoka marehemu.
Alisema Mwili wa Dk. Mgimwa unatarajia kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (Terminal II) jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Januari 4, 2014 majira ya saa saba mchana na utapokelewa na ndugu, viongozi wa Serikali, Wananchi pamoja na kamati husika.
Alisema mwili huo utaifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo hadi Jumapili ya Januari 5, ambapo utapelekwa katika Ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya kuombewa na baadaye salamu za mwisho kabla ya kusafirishwa kuelekea Mkoani Iringa kwa ajili ya mazishi.
“…Mwili utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere-Terminal I saa nane mchana kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea Iringa. Mwili utawasili Iringa Uwanja wa Ndege wa Nduli saa kumi alasiri na kupelekwa katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo kwa ajili ya kuagwa,” alisema Waziri Lukuvi.
Aidha alisema marehemu waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa anatarajiwa kuzikwa Kijijini Magunga Jumatatu ya Januari 6, 2014 saa sita mchana.