Na Aron Msigwa, Dar es Salaam
SERIKALI imewataka watendaji na wamiliki wa makampuni kutoka ndani na nje nchi kuacha tabia ya kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wageni na badala yake wawatumie vijana wa kitanzania wanaohitimu masomo katika vyuo mbalimbali hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Waziri wa Viwanda Biashara, Dk. Abdallah Kigoda wakati akizungumza na wahitimu 3363 wa fani mbalimbali wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam waliohudhuria mahafali ya 49 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Alisema Tanzania ina vijana wengi wenye kukidhi viwango na uwezo wa kutekeleza majukumu ya Uhasibu, Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko, Manunuzi na Ugavi, Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ufanisi mkubwa kutokana na mafunzo waliyopewa katika vyuo na taasisi mbalimbali hapa nchini.
“Tanzania tunao vijana bora na wenye kukidhi viwango wanaohitimu kila mwaka,suala la kutoa visingizio kuwa hatuna wataalam na makampuni haya kuajiri wageni katika nafasi za kawaida na ngazi za utawala mimi sikubaliani nalo, nakemea tabia hii,” alisisitiza Dk. Kigoda.
Alifafanua kuwa Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ukosefu wa ajira lililopo hapa nchini kwa kujenga na kuandaa mazingira wezeshi ya kukuza utengenezaji wa ajira za kujiajiri na kuajiriwa kwa kuendeleza sekta binafsi katika eneo la Kilimo, Sekta ya Viwanda na Biashara hususan ujasiriamali mdogo na wa kati.
Ameeleza kuwa serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa wahitimu hao kujiajiri wenyewe kwa kuratibu mfumo wake wa kodi na tozo mbalimbali, kuangalia hatua za utoaji wa leseni na usajili wa biashara, kushughulikia tatizo la uhaba wa mikopo na riba zinazotolewa kwa wale wanaotumia mikopo kama mitaji pamoja na kushughulikia suala la mikataba inayoandaliwa na makampuni ambayo mara nyingi inawakosesha vijana fursa ya kupata ajira.
Ametoa wito kwa wahitimu hao kuwa wajasiri na wenye moyo wa kuthubutu wa kutumia taaluma na mafunzo waliyopata kuleta mabadiliko na maendeleo nchini huku akiwataka wahitimu hao kuepuka tabia ya uzembe, uvivu na Rushwa pindi watakapoingia kwenye ajira.
Kuhusu uboreshaji chuo hicho Dk. Kigoda amesema Serikali inaendelea kukijengea uwezo chuo hicho kwa kuimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa hususan matumizi ya mifumo ya kompyuta na mawasiliano (ICT) ili kiweze kushindana na vyuo vya kigeni vilivyoanzisha kampasi zao hapa nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga akizungumzia mahafali hayo ya 49 ya chuo hicho amesema kuwa yanakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho. Alisema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 mafanikio mbalimbali yamepatikana yakiwemo ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kujiunga na masomo hadi kufikia kutoka 25 pindi chuo kinaanzishwa hadi 14000 wa sasa, ongezeko la kampasi kutoka 1 hadi kufikia 4.
Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo kutoka 1iliyokuwepo mwaka 1965 hadi 6 zilizopo sasa na ongezeko la wakufunzi wenye shahada ya uzamivu (PhD). Prof. Luhanga amefafanua kuwa chuo hicho sasa kimeanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine vilivyo nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Maastricht cha Uholanzi, Chuo Kikuu cha Stockholm cha Sweeden na Chuo Kikuu cha Eastern Finland ambacho kimeshirikiana na CBE kutoa mafunzo ya shahada ya uzamivu kwa nchi za SADC.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema akiwakaribisha wahitimu, wadau mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo hicho waliohudhuria mahafali hayo amesema kuwa chuo chake kimepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965 ikiwemo ongezeko la idadi ya wanafunzi wa kike wanaohitimu chuoni hapo hadi kufikia asilimia 48 kwa mwaka 2014.
Alisema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wataalam wengi katika fani za Uhasibu, Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko, Manunuzi na Ugavi, Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameweza kuhitimu na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.