Waziri Amuagiza Mkuu wa Wilaya Kuziba Nyufa za Tetemeko la Ardhi

Tetemeko la ardhi lilivyoathiri baadhi ya majengo Mkoani Kagera

Tetemeko la ardhi lilivyoathiri baadhi ya majengo Mkoani Kagera

 

Na Beatrice Lyimo, MAELEZO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera kufanya ukarabati wa haraka wa kuziba nyufa zilizotokea katika taasisi za Serikali zilizoathirika kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea hivi karibuni Mkoani humo.

Waziri Mhagama aliyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kukagua taasisi mbalimbali za Serikali zilizoathirika kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani humo tarehe 10 Septemba mwaka huu.

Katika ziara hiyo, Waziri Mhagama alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo kutoa misaada kwa waathirika waliofanyiwa tathmini ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali Denice Filangali Mwila alisema kuwa Ofisi yake imeshaanza kuwaga baadhi ya maturubai na chakula ikiwemo sukari kwa waathirika wa tetemeko hilo.

Aidha Waziri Mhagama pia alitembelea Shule ya Msingi Byeju iliyopo Wilayani humo ili kujionea baadhi ya vyoo na madarasa ya shule ambayo yalivyoathirika na tetemeko hilo na kuagiza ukarabati wa miundombinu hiyo kuanza mara moja.