Wazazi watakiwa kujipanga katika malezi

WAZAZI wametakiwa kuwalea watoto katika maadili mema pamoja na kuwajengea misingi imara ya kielimu kutokana na ukweli kwamba elimu ndio urithi kipekee ambao mzazi anaweza kumwachia mwanae.

Rai hiyo ilitolewa na vijana wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)Dayosisi ya Kaskazini usharika wa Moshi Pasua, wakati wa kufunga juma la vijana ambalo huadhimishwa mwezi julai kila mwaka.
Vijana hao walisema ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha anatimiza wajibu wake wa malezi bora kwa watoto ikiwemo kuwapatia elimu, hatua ambayo itawawezesha kukabiliana na changamoto za kimaisha pindi watakapofikia kujitegemea.
Akizungumza Bw. Nimrod Kimaro alisema kuwajengea watoto misingi thabiti ya elimu huwafanya kuwa imara na kujiamini hivyo kuongeza idadi ya wasomi hapa nchini na kupunguza tatizo la watoto wa mitaani ambalo kwa kiasi kikubwa linachangiwa na mimba zisizotarajiwa.

Bw. Kimaro alisema kumekuwepo na wazazi wengi ambao wamebweteka katika malezi, hali ambayo inachangia vijana kuharibikiwa kimaisha ikiwa ni pamoja na kuijiingiza katika vitendo viovu ikiwemo uvutaji wa madawa ya Kulevya na Ngono zembe.
“Wazazi wengi wamekuwa chanzo cha sisi vijana kuharibikiwa kimaisha kwani wamejisahau katika malezi na hali hii inasababisha kuwepo kwa kundi la vijana lisilo la maadili ambako ndiko kunapatikana vibaka,wezi na walevi wa kupindukia na baada ya hapo mimba za zisizotarajiwa,mimba za utotoni na hata maambukizi ya ugonjwa hatari wa ukimwi”alisema Kimaro..

Alisema ni vema wazazi wakajijengea tabia ya kuwa karibu na watoto
wao ili kuweza kuwaepushia matatizo ambayo hukumbana nayo pindi wawapo
mashuleni kwa madai kuwa watoto wengi hupoteza mwelekeo wa kimaisha
kutokana na wazazi wao kutojipanga vizuri katika malezi.

Akizungumza katika kilele hicho cha juma la vijana mchungaji kiongozi wa Usharika wa Moshi Pasua Bw. Elirehema Silaa aliwataka vijana kujitambua na kujijengea tabia ya kujishughulisha na kazi mbalimbali za kimaendeleo hatua ambayo itawasaidia kuondokana na hali ya utegemezi katika jamii.