Wazazi Waliogoma Kusomesha Wanafunzi Kusakwa Rombo

Wanafunzi Nduweni Sekondari Rombo

Wanafunzi Nduweni Sekondari Rombo

SERIKALI wilayani Rombo imetangaza kuanza msako mkali wa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wazazi/walezi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2014 ambao bado watoto wao hawajaripoti shuleni hadi sasa.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Elinas Pallengyo ameyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani ambapo alisema kuwa zoezi la msako huo linatarajia kuanza muda wowote kuanzia sasa.

Alisema taarifa walizonazo ni kwamba kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini hadi sasa bado hawajaripoti shuleni, hivyo serikali haitalifumbia macho suala hilo kwani wamejipanga kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni kwa haraka iwezekanavyo.

Aidha alisema wameamua kufanya hivyo baada ya kubaini wazazi wengi wamekataa kuwapeleka watoto mao shuleni kwa kisingizio cha kutokua na fedha za kuwalipia gharama mbalimbali zinazotakiwa shuleni.

Alisema kwa mwaka jana (2013) zaid ya wanafunzi 1500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza hawakuripoti shuleni jambo ambalo linakwamisha watoto kukosa haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kupata elimu.

Aidha Pallengyo aliongeza kuwa uongozi wake umesikitishwa na matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2013, ambapo Wilaya ya Rombo ilishika nafasi ya mwisho katika Mkoa wa Kilimanjaro na kushindwa kufikia viwango vya alama za mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).

Alisema ipo haja ya wadau wote wa elimu kukutana ili kujadili mambo yaliochangia Wilaya ya Rombo kushika nafasi ya mwisho ili suala hilo lipatiwe ufumbuzi wa haraka.