BAADHI ya wanafunzi wa kike katika Shule ya Msingi Nachitulo Wilayani Newala wamewataka wazazi kuacha tabia ya kuwabagua watoto wa kike kielimu kwani kufanya hivyo ni kumnyanyasa mtoto wa kike kijinsia.
Wanafunzi hao walitoa kilio hicho hivi karibuni katika mjadala uliofanyika kwenye shule hiyo uliokuwa ukijadili vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na uelewa wa vitendo hivyo kwa watoto ili
kuweza kukabiliana navyo.
Mwanafunzi Sofia Damian wa darasa la tano ‘B’ Shule ya Msingi Nachitulo akizungumza katika mjadala huo aliwaomba wazazi kuacha tabia ya kufanya ubaguzi wa kumjali zaidi mtoto wa kiume kielimu na kumsahau yule wa kike kwani kitendo hicho ni ukatili wa kijinsia.
Alisema baadhi ya wazazi eneo hilo wamekuwa wakibagua watoto kwa kumjali zaidi wa kiume na kuwaacha wa kike ni ubaguzi mbaya. “…Kitendo cha kufanya ubaguzi wa elimu katika familia kwa mtoto wa kike na kiume ni unyanyasaji wa kijinsia…yaani kumpeleka mtoto wa kiume shuleni na kumuacha wa kike nyumbaji hilo ni unyanyasaji,” alisema Sofia Damian.
Kwa upande wake Sharifa Bakari toka darasa la sita ‘A’ katika shule hiyo alisema ubaguzi wa mtoto
wa kike umekua ukianzia ngazi za familia kwa watoto wa kike kuwa na kazi nyingi nyumbani zaidi ya mtoto wa kiume kitendo ambacho kinatakiwa kipigwe vita.
Mwanafunzi wa darasa la sita ‘A’ katika shule hiyo, Mwanahamisi Said aliwataka baadhi ya wazazi na walezi kuacha utaratibu wa kumlazimisha mtoto wa kike kuolewa kwa taamaa ya mali (ndoa za utotoni), kwani kitendo hicho pia ni ukatili wa kijinsia. “..Hata kitendo cha mtu mzima kumlazimisha mwanafunzi kufanya naye mapenzi ni ukatili wa kijinsia,” alisema Mwanahamisi.
Akizungumza mwongozaji wa mjadala huo, Suzan Charles kutoka Kituo cha Usuluhishi (CRC) kilichopo chini ya Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) aliainisha matukio ya ukatili wa kijinsia yanayowapata watoto na kutoa elimu ya kukabiliana nayo kwao, ikiwa ni pamoja na wao kutoa taarifa
mapema sehemu husika endapo watatokewa na hali kama hizo.
Akizungumza awali kabla ya mjadala huo, Mwalimu wa Malezi wa Shule ya Msingi Nachitulo, Blandina
Luwongo alisema shule hiyo imefanikiwa kupiga vita vitendo vyovyote vya ukatili wa kijinsia kwa
watoto kwa kutumia mradi wa elimisha rika jambo ambalo limeondoa kabisa matukio ya mimba kwa wanafunzi.
“…Katika shule yetu hata matukio ya wanafunzi kutiwa mimba hayapo kwa sasa baada ya elimu ya uelimishaji rika kutolewa kwa jamii, wanafunzi na walimu eneo hili. Hata hivyo anabainisha ili kutokomeza kabisa matukio ya unyanyasaji elimu ya kukabiliana na vitendo hivi kwa jamii haina
budi kutolewa kiufasaha na kuacha kujikita kwenye adhabu kwa wakosaji.” Anasema Bi. Luwongo.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com