Waagiza Sub Marine kutoa Afrika Kusini
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KAZI ya kuopoa miili ya watu walionasa kwenye mabaki ya Meli ya Mv. Spice Islanders lililokuwa likifanywa kwa pamoja na wazamiaji kutoka nchini Afrika ya Kusini na Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania hatimaye imeshindikana.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu imezipata leo toka kwa Ofisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, kazi hiyo imeshindikana kutokana na kuchafuka kwa hali ya bahari na kina kirefu ilichozama meli hiyo kwa sasa hivyo kuwashinda wazamiaji kutoka Afrika ya Kusini.
Inspekta Mhina amesema uamuzi wa kusitisha zoezi hilo umetangazwa na Kamanda wa Operesheni hiyo kutoka nchini Afrika ya Kusini, Bw. Wayne Combrink, ambapo amesema, wazamiaji wake na wale wa nchini wameshindwa kuifikia meli hiyo baada ya kubaini kuwa kwa sasa ipo umbali wa zaidi ya mita 300 chini ya Bahari-huku uwezo wa wazamiaji hao ni kina kisichozidi mita 54 tu.
“Kwa hiyo kutokana na hali hiyo, Kamanda huyo amesema wameagiza meli maalumu ya Sub Marine kutoka nchini Afrika ya Kusini ili kuja kukamilisha zoezi hilo ambalo amesema lisingewezekana kutekelezwa kwa wazamiaji wenye zana za kawaida bila chombo hicho,” alisema Mhina.
Wazamiaji hao Afarika Kusini waliwasili Zanzibar usiku wa Septemba 13 wakiwa na kundi la watu 16 wakiwemo madaktari wanne pamoja na vifaa vya kisasa wakidhani kina kilichozama meli hiyo kingekuwa chini ya mita 54.