Wazamiaji 130 Wafa Majini Wakielekea Ulaya

Baadhi ya miili ya waamiaji baada ya kutolewa majini.

Baadhi ya miili ya waamiaji baada ya kutolewa majini.

MAOFISA katika Kisiwa cha Sicily cha Bahari ya Meditarenia wamesema wamepata maiti 130 baada ya mashua iliyokuwa imewabeba wahamiaji 500 wa Kiafrika kushika moto na kuzama katika Kisiwa cha Lampedusa.

Boti hiyo ilikuwa safarini kuelekea Ulaya lakini ikazama katika kisiwa cha Lampedusa katika pwani ya Utaliana. Taarifa zinasema miili 103 imepatikana baharini huku mingine zaidi kupatikana ndani ya boti lililozama.

Taarifa zaidi zinasema abiria waliamua kujirusha baharini wakati moto ulipozuka ndani ya boti walilokuwa wakisafiria. Hata hivyo zaidi ya wahamiaji 150 wameokolewa katika ajali hiyo. Wengi wa wahamiaji hao walikuwa raia wa Eritrea na Somalia, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Shughuli kubwa ya uokozi ingali inaendelea kuwatafuta manusura kwani inahofiwa mamia zaidi huenda wamefariki kutokana na ajali hiyo. Meya wa mji huo anasema kuwa walionusurika wako hatika hali ya mshutuko na walimwambia kuwa moto mdogo uliwashwa baada ya meli kukwama na lengo lilikuwa kuitisha msaada.

Lakini alisema kuwa moto ulisambaa kupita kiasi na ikawa vigumu kuudhibiti. Kisiwa cha Lampedusa kiko kati ya Tunisia na Sicily na kimekuwa kiingilio kikuu cha wahamiaji kuingia barani Ulaya.
-BBC