Wawakilishi Pemba Watakiwa Kuwekeza Katika Elimu

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi” (aliyesimama) akizungumza.

 

Na Is-haka Omar, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka Wabunge na Wawakilishi wa Pemba kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuwasaidia vijana wanaosoma kwenye shule na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo katika kisiwa hicho. Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi” katika mwendelezo wa ziara yake Pemba wakati akikagua ujenzi wa shule ya Msingi na Sekondari ya Kwale Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema viongozi hao pamoja na majukumu waliyokuwanayo wanatakiwa kubuni miradi itakayosaidia kuinua viwango vya elimu kwa vijana mbali mbali waliopo katika majimbo hayo ili waweze kupata taaluma zinakazowasaidia kujiajiri wenyewe. Alisema endapo kila jimbo litakuwa na wataalamu mbali mbali waliosomeshwa na viongozi wa majimbo hatua hiyo itaongeza kasi ya maendeleo kwa kupata wataalamu wa fani mbali mbali watakaohudumu kwenye sekta za umma na binafsi katika majimbo hayo.

Sambamba na hayo aliwaagiza Wabunge na wawakilishi hao kuongeza kasi katika kutatua kero zinazowakabili wananchi ili kwenda sambamba na matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Dkt. Mabodi alisema viongozi hao wanatakiwa kuwa wa kwanza kuratibu changamoto zinazowakabili wananchi kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kama walivyowaahidi wananchi hao katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

“Elimu ndio silaha pekee ya kukuza maendeleo ya nchi yetu pia tutakapokuwa na wasomi wengi wazawa ndio watakaoweza kupanga mikakati endelevu ya kukuza uchumi wa taifa letu.”, alieleza Dkt. Mabodi.

Pamoja na hayo amewapongeza wananchi wa shehia ya Kwale Kisiwani Pemba kwa uzalendo wao wa kushiriki katika shughuli za kijamii zikiwemo ujenzi wa Skuli ya Kwale ambayo kwa sasa wanasoma watoto wa shehia hiyo na vitongoji vyake. Pia aliwaomba wananchi wa kisiwa cha Pemba kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein Pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusimamia vizuri fursa za kimaendeleo na kuimarika uchumi wa nchi zote mbili.

Kupitia ziara hiyo Dkt. Mabodi kwa niaba ya CCM Zanzibar alichangia shilingi milioni tatu kwa lengo la kusaidia ujenzi wa madarasa ya Shule ya Kwale.