Wauzaji petroli, dizeli waiweka pabaya Serikali ya JK


Rais Kikwete.

WAFANYABIASHARA wa nishati za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini, sasa wanaiweka pabaya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kile kuonekana kugomea uamuzi uliotolewa juzi wa kushusha bei za nishati hiyo.

Uchunguzi uliofanywa a waandishi wa mtandao huu jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa, umebaini kuwa wafanyabiashara wengi wamegoma kuendelea kutoa huduma hiyo kwa wananchi jambo ambalo limekuwa kero.

Taarifa zilizotufikia kutoka mikoa ya Mbeya, Rukwa, Morogoro na Dar es Salaam yenyewe baadhi ya wauzaji waligoma kiaina kutoa huduma hiyo huku kila mmoja akiwa na sababu yake.

Hata hivyo vituo ambavyo vilitoa huduma hiyo navyo havikuuza kwa bei ambazo zilipangwa na Serikali jambo ambalo lilikuwa na usumbufu mkubwa kwa wananchi hasa wanaotegemea nishati ya vyombo vya moto.

Baadhi ya wauzaji waliogoma walisingizia kuharibika kwa mashine za kusukuma mafuta, vituo kukosa umeme na vituo vingine kueleza kutokuwa na mafuta kwa ya kuuza takribani wiki moja kabla ya tamko la Serikali.

Taarifa zinasema vituo vyote vya Mji wa Sumbawanga, Nkasi na Mpanda kwa siku nzima jana havikutoa huduma hiyo hali ambayo imesababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa bidhaa hiyo eneo hilo.

Hali hiyo ya mgomo kwa Sumbawanga ilitoa mwanya kwa baadhi ya watu binafsi kuanza kuuza kinyemela bidhaa hizo, ambapo mafuta ya taa yaliuzwa kati ya Sh. 2700 hadi 3000, Petroli Sh. 5000 hadi 6000 huku dizeli ikiuzwa kwa bei kama hiyo kwa lita.

“Si kwamba hawauzi mafuta kwa sababu wanazozitoa, huu ni uongo hawa wamegomea uamuzi wa Serikali ambayo imeshusha bei ya nishati hizo kuanzia leo (jana),” alisema dereva mmoja mjini Sumbawanga pembeni ya kituo kimoja cha mafuta.

Serikali jana kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati za Maji na Mafuta (EWURA) ilitangaza kushusha bei za nishati za mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa kwa kile kudai yamekuwa yakipanda tofauti na uwiano.

Kufanyika kwa mgomo baridi huo baadhi ya mikoa kumeiweka pabaya Serikali, ikiwa bado kwenye kipindi kigumu ambapo upatikanaji wa nishati ya umeme umekuwa ukisumbua na sasa kuingia kwa nishati za mafuta pia.