Waumini Kanisa la Kikristo kujengewa uwezo

Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA, John Mnyika miongoni mwa wageni waalikwa katika mkutano huo.

Na Tiganya Vincent, MAELEZO- Dar es Salaam

WASHIRIKI zaidi ya 200 wa Kanisa la Kristo kutoka sehemu mbalimbali nchini wanatarajia kukutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujengewa uwezo kuanzia Jumatatu hadi Jumatano. Hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo kwa ajili kuwafanya waondokane na utegemezi.

Kauli hiyo itolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Kanisa la Kristo Magomeni Mwembechai Elikana Balandya wakati akiongea na waandishi wa habari. Waumuni hao wanatarajia kutoka Kanisa la Kristo la Temeke (Mwembeyanga), Mbagala Rangi Tatu, Keko, Luhanga, Mjimwema, Mlandizi, Msasani, Banana, Kitunda, Kigogo, Kingugi, Singida, Arusha na Mbeya.

Alisema kauli mbiu ya mkutano huo ni kujenga uwezo wa waumini na makanisa ili kuondokana na utegemezi. Balandya aliongeza kuwa Mkutano huu utaendeshwa kwa ushirikiano na Kanisa la Kristo la River-Road, Georgia (Marekani) pamoja na Kanisa la Kristo la Soweto (Afrika Kusini).

Aidha, miongoni mwa washiriki hao kutoka Marekani na Afrika kusini kuna timu ya madaktari itakayotoa huduma ya ushauri wa kitabibu na masuala mbali-mbali ya afya kwa jamii inayoizunguka Kanisa.

Matibabu hayoni ni pamoja na namna ya kujikinga na shinikizo la damu (blood pressure monitoring), uchunguzi wa sukari damuni (blood glucose tests), uchunguzi wa wingi wa mafuta mwilini (blood cholesterol tests), uchunguzi wa uzito unaostahili mwilini (body mass index), na elimu kuhusu saratani, mlango wa kizazi (cervix), matiti, malezi bora ya watoto, na chanjo muhimu.

Alisema kuwa katika mkutano huo wageni waalikwa wanaotarajiwa kuhudhuria hafla ya ufunguzi wa mkutano ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (Mgeni rasmi), John Mnyika (Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA) na Idd Azzan (Mbunge wa Jimbo la Kinondoni-CCM)