Watumishi wa Umma Watakiwa Kukuza Uchumi

Waziri Kombani amesema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa siku mbili unaohusu majukumu ya watumishi wa Umma katika kutekeleza  Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano.

Na Georgina Misama-Maelezo

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Manejimenti  ya Utumishi wa Umma Celina Kombani amewataka watumishi wa Umma kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kukuza uchumi wa nchi.

Waziri Kombani amesema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa siku mbili unaohusu majukumu ya watumishi wa Umma katika kutekeleza  Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano.

Alisema ubora au udhaifu wa utendaji wa serikali yoyote unahusishwa  na ubora wa watumishi wa Umma.

“Uchumi hauwezi kukua bila watumishi wa umma kufanya kazi vizuri, katika kukuza uchumi tunategemea,kukua kwa uchumi pia kunategemea watumishi wa umma,” alisema Waziri Kombani.

Waziri Kombani alisema kwa kipindi cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania bara, Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo, ingawa inakabiliwa na changamoto mbali mbali.

Pamoja na changamoto hizo, Waziri Kombani amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbali mbali ikiwemo, kupitia na kutafakari jinsi ya kufikia malengo ya maendeleo yake kwa haraka  zaidi
 Alisema changomoto zilizopo katika utumishi huo ni kuwa huduma zinawafikia wananchi kwa polepole, zisizo na ubora mfano kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaondikishwa katika shule ya msingi na sekondari, lakini kuna tatizo la ubora wa elimu.

“Tunapo sema uchumi wa nchi inatakiwa kumwangalia mtu wa ngazi za chini. Hivyo mkutano huu utakuwa unajadili changamoto zilizopo na nini kifanyike,” alisema.

Aidha aliongeza kuwa wakati mwingine wananchi wanalalamikia kuwepo kwa vitendo vya rushwa.

Hata hivyo  Waziri Kombani ametoa wito  kwa viongozi kutafuta majibu ya changamoto zilizopo, ikiwemo ongozeko la idadi ya watu, matumizi ya rasilimali na matumizi bora ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mkutano huo wa siku mbili, unawashirikisha manaibu  makatibu wakuu kutoka wizara mbalimbali, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa taasisi za elimu ya juu , sekta binafsi na  wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania.