Watumishi wa Serikali wameaswa kuwa na nidhamu ya matumizi bora ya rasilimali fedha ili kuleta ufanisi na maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wa mkoani Lindi na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile alipokuwa akiongea na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya wafanyakazi Hazina Ndogo hivi karibuni mkoani Lindi .
“Matumizi ya fedha ni lazima yaende sawa na ukusanyaji wa mapato yakiwemo mapato yasiyo kuwa na kodi, inabidi Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri kuzingatia umuhimu hasa katika kusimamia mapato na matumizi ya Serikali kwa kila kiasi kidogo kinachopatikana” alisema Dkt. Likwelile.
Dkt. Likwelile amesema kuwa Serikali inafanya mapitio ya Mkakati wa Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA) na kuhakikisha kuwa changamoto zilizokuwepo awali zinapatiwa ufumbuzi ili kuleta tija na ufanisi.
Kwa upande wake Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Lindi alipokuwa akimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa niaba ya watumishi wa Hazina Ndogo alisema kuwa watajitahidi kuzingatia maelekezo aliyoyatoa ili kuleta tija na ufanisi katika sehemu zao za kazi.