‘Watumishi umma wala rushwa ni watumwa’

WATUMISHU wa umma wanaokumbatia rushwa wamefananishwa na watumwa wanaoabudu wenye mali.
“Mtumishi wa umma mla rushwa ni mtumwa anayeabudu wenye mali na kamwe hawezi kuwa na ufanisi kazini”, alisema Emmanuel Mlelwa, Kaimu Mkurungenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Mlelwa alizungumza hayo wakati wa semina ya siku moja iliyoandaliwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru) kwa wakuu wa idara wa halmashauri hiyo.
Alisema rushwa ni adui wa haki na maendeleo hivyo ni vyema wakuu wote wa idara na kila mtumishi kuhakikisha anaepukana nayo.
Kaimu mkurugenzi huyo aliwataka wakuu wa idara na washiriki wa semina hiyo kuhakikisha wanakwenda kutekeleza kwa vitendo yale yote watakayojifunza na kuwahimiza kupeleka elimu hiyo kwa watumishi wengine waliopo chini yao.
Semina hiyo ilikuwa ikiwafunza watendaji hao wa umma sheria, madhara ya rushwa na namna ya kuepukana nayo.
Mkuu wa Takukuru wa Wilaya ya Ludewa, Edings Mwakambonja alieleza madhara makubwa ya rushwa kuwa ni pamoja na kusababisha vifo, kushuka kwa pato la taifa, kukosekana kwa haki, kuongezeka kwa umaskini, kupata viongozi wasio waadilifu na mmomonyoko wa maadili kwa jamii.
Akitoa mada katika semina hiyo, Mwakambonja alisema rushwa zimegawanyika katika makundi mawili; rushwa ndogo inayoendeshwa na watumishi wa kada ya chini ambayo madhara yake kijamii humpata mtu mmoja mmoja zaidi.
Nyingine ni rushwa kubwa inayoendeshwa na watumishi wa kada ya juu ambayo inahusisha kiasi kikubwa cha fedha, ambayo pia huwahusisha wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa.
Alisema rushwa kubwa hushawishi hata kubadilishwa kwa sera na taratibu halali kwa lengo ya kupata upenyo rahisi kwa manufaa ya wafanyabiashara na wawekezaji.
Wakuu wa idara wa wilaya hiyo wakitoa maoni yao kuhusu mafanikio ya semina hiyo walieleza kupata elimu kubwa juu ya makatazo ya rushwa, njia za kuiepuka na zaidi kupata mwanga wa namna ya kuwafundisha watumishi wengine ubaya wa rushwa.