Watuhumiwa wa EPA wawili waenda jela miaka 5

Na Mwandishi Wetu

WATUHUMIWA Farijala Hussein na binamu yake Rajabu Maranda wa kesi ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wamehukumiwa kwenda jela miaka mitano.

Maranda ambaye ni mfanyabiashara na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mpwa wake, Hussein walihukumiwa kifungo hicho jana jijini Dar es Salaam katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kupatikana na hatia katika makosa sita.

Umati wa watu hasa ndugu wa watuhumiwa hawakuamini macho yao baada ya kumalizika kwa kesi hiyo na watuhumiwa kukamatwa na polisi kwenda kutumikia adhabu zao.

Watuhumiwa hao pia wametakiwa kufilisiwa mali zao ili kuhakikisha wanalipa kiasi cha Sh. bilioni 1.8 ambazo wanadaiwa kukwapua kijanja katika kesi za EPA zilizofunguliwa mfululizo mwaka 2008 chini ya msaada wa waendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Hata hivyo hii ni kesi pekee kati ya kesi hizo ambayo imetolewa hukumu baada ya kusikilizwa ushahidi wa pande zote mbili. Pamoja na hayo tayari wakili aliyekuwa akiwatetea watuhumiwa hao ameonesha nia ya kukata rufaa na amevieleza vyombo vya habari mara baada ya hukumu kusomwa kuwa atasoma kwa makini hukumu na kuangalia hoja za kupinga hukumu hiyo.

Washitakiwa hao walikuwa wakituhumiwa kula njama, kughushi, wizi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia ingizo la fedha kwa njia ya udanyifu kiasi cha Sh 1,864,949,294.45, mali ya Benki Kuu (BoT) walipojaribu kuonesha kuwa kampuni yao ya Kiloloma Brothers ilipewa idhini ya kukusanya deni la Kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India.

Maranda na mwenzake Farijala pia bado wanakabiliwa na kesi zingine za aina hiyo katika mahakama hiyo ambazo zipo katika hatua mbalimbali na huenda wakaendelea kuwa wafungwa watuhumiwa huku wakitumikia adhabu zao. Kesi nyingine zinazowakabili washitakiwa hao zimepangiwa kusikilizwa Mei 27 mwaka huu.