WAKATI Serikali ya Tanzania imeanza kuwafikisha mahakamani baadhi ya maafisa wanaotuhumiwa kuhusika na gawio la fedha kutoka akaunti ya Tegeta ESCROW, Chama tawala nchini humo CCM, kimetoa kauli ya kuwachukulia hatua, makada wake wanaohusishwa na kashfa hiyo.
Suala la kashfa ya akaunti ya mabilioni ya fedha yaliyochotwa kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, si tu imekichafua chama tawala nchini humo kutokana na baadhi ya wanachama wake kutajwa kuhusika na kashfa hiyo, bali pia serikali ilijikuta wakati wa sakata hilo ikisitishiwa msaada wa fedha katika bajeti yake.
Baadhi ya maafisa wa serikali ambao wamefikishwa jana mahakamani kwa tuhuma za kuingiziwa mamilioni ya fedha hizo katika akaunti zao ni Mkurugenzi Huduma za sheria katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi Rugonzibwa Mujunangoma pamoja na Mhandisi Mfawidhi wa Wakala wa Umeme Vijijini Theophilo Bwakea.
Wakati vuguvugu la uchaguzi mkuu nchini Tanzania utakaofanyika baadaye mwaka huu likikaribia, uongozi wa chama hicho umeendelea kuwaonya makada wake sita, ambao wamepewa adhabu kwa madai ya kuanza kampeni za kuwania Urais, kabla ya wakati, wanaweza kuongezewa adhabu itakayowasababishia kuondolewa katika kinyang’anyiro hicho, iwapo itathibitika kwamba walikuwa wakiendelea na kampeni hizo wakati wakitumikia adhabu.