Watu 92 wauwawa mashambulio ya kigaidi Norway


Majeruhi wakitibiwa barabarani katika mji mkuu wa Norway, Oslo

POLISI nchini Norway, imearifu kwamba watu wasiopungua 92 wameuawa kutokana na mashambulio mawili ya kigaidi. Kati ya hao, 84 waliuawa kwenye kambi ya vijana ya chama cha Social Demokratik iiyopo katika kisiwa cha Utoya karibu na mji Mkuu wa Norway, Oslo. Watu hao walipigwa risasi na mtu aliejifanya kuwa polisi.

Mshambuliaji huyo aliingia katika kisiwa hicho jioni ya jana na alianza kufyatua risasi. Polisi walimkamata mtu huyo mwenye umri wa miaka 32, baada ya muda wa nusu saa. Polisi inatuhumu kuwa mtu huyo ndie pia alielifanya shambulio la bomu mjini Oslo. Polisi sasa, inamsaka mtu wa pili anaetuhumiwa kuhusika na mashambulio hayo. Majeruhi waliofyatuliwa risasi katika kisiwa cha Utoya nchini Norway

Muda wa saa 2 kabla ya mauaji kufanyika kwenye kisiwa cha Utoya, watu 7 waliuawa mjini Oslo, baada ya bomu kulipuka kwenye kitongoji cha serikali .Bomu hilo lililipuka karibu na ofisi ya Waziri Mkuu Jens Stoltenberg.

Wakati huo huo mtu aliekuwa na kisu akiwa karibu na waziri Mkuu huyo amekamatwa na polisi.Hapa nchini Ujerumani, Waziri wa mambo ya nje Guido Westerwelle pia ameyalaani vikali mashambulio hayo ya kigaidi.
-DW