WANAHARAKATI wa kutetea haki za binadamu nchini Syria wanasema maofisa wa vikosi vya usalama wamewaua watu saba, akiwemo mwanamke mmoja aliyekufa kutokana na mateso. Watu wanne waliuwawa katika Mji wa Homs katikati ya Syria na waandamanaji wawili wakauwawa katika kitongoji cha Talbisseh, Kaskazini mwa mji huo. Zaidi ya watu 150 wamekamatwa katika saa 24 zilizopita kwenye kitongoji kimoja cha Mji Mkuu Damascus.
Wanaharakati pia wanasema vikosi vya usalama vinaendelea na operesheni yao dhidi ya waandamanaji katika sehemu mbalimbali ya nchi, na vifaru vinatumika katika baadhi ya maeneo hayo. Marekani na Umoja wa Ulaya zimewasilisha rasimu ya azimio katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutaka vikwazo vikali dhidi ya rais wa Syria, Bashar al Assad na familia yake. Marufuku ya kuagiza mafuta ya Syria katika nchi za Umoja wa Ulaya inatarajiwa kupitishwa wiki ijayo.
-WD