WATU saba wameuawa kwa kupigwa risasi katika shambulizi karibu na msikiti Kaskazini Mashariki mwa Kenya, karibu na mpaka na Somalia. Wanakijiji waliambia BBC kuwa watu kumi waliokuwa wamejihami waliwashambulia kwa bunduki watu hao wakati walipokuwa wanaondoka msikitini mapema asubuhi.
Taarifa zinazohusiana
Mwanzo wanaume watano waliuawa na kisha wanawake wawili waliosikia milio ya risasi walipofika kuchunguza, nao pia wakauawa. Shambulio linafanyika chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi kufanyika katika eneo mojawapo ambapo usalama ni tatizo kubwa.
Wenyeji wa kijiji cha Malaley wanasema kuwa hakuna kilichoibiwa kwani washambuliaji walitoroka punde baada ya shambulizi. Kijiji hicho kiko umbali wa kilomita 45 kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab ambayo ni makao kwa wakimbizi zaidi ya laki tano, waliotoroka vita nchini Somalia.
Katika mwaka mmoja uliopita, eneo hilo limekumbwa na mashambulizi ambayo yamelaumiwa kwa kundi la wapiganaji wa kiisilamu Al Shabaab. Al-Shabab iliahidi kulipiza kisasi wakati wanajeshi wa Kenya walipokwenda Somalia kupambana nao, mwezi Oktoba mwaka 2011 kama juhudi za kusaidia wanajeshi wa muungano wa Afrika.
-BBC