Watoto Wenye Mahitaji Maalum Wanahitaji Ulinzi na Mapenzi…!

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akishangiliwa na watoto wadogo (chekechea) wa shule ya awali ya Carlton iliyoko Colombo, nchini Sri lanka wakati Mama Salma na wake wa Marais na Wakuu wa Nchi za Madola walipotembelea shule hiyo tarehe 16.11.2013.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akishangiliwa na watoto wadogo (chekechea) wa shule ya awali ya Carlton iliyoko Colombo, nchini Sri lanka wakati Mama Salma na wake wa Marais na Wakuu wa Nchi za Madola walipotembelea shule hiyo tarehe 16.11.2013.

Na Anna Nkinda – Colombo, Sri Lanka

WATOTO wenye mahitaji maalum wanahitaji kupata ulinzi na mapenzi ya mara kwa mara kutoka kwa walezi na jamii inayowazunguka ikiwa ni pamoja na kupata nafasi ya kwenda shule kwani wengi wao wananyimwa fursa hiyo ukilinganisha na watoto wengine. Aidha mtoto akipata elimu ni moja ya hatua ya mwanzo katika maendeleo ya taifa kwani baada ya kuelimika atakuwa na ujuzi wa kitaaluma, kiteknolojia na  raia mwenye kufuata maadili ya nchi yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shule ya awali ya Carlton inayoongozwa na Mke wa Rais wa Sri Lanka Mama Shiranthi Wickremasinghe Rajapaksa wakati wake wa Marais na wakuu wa nchi na Serikali walipotembelea shule hiyo iliyopo mjini Colombo jana ilionyesha kuwa shule hiyo inamtazamo wa kutoa elimu kwa mtoto.

Elimu ya shule hiyo ambayo hutolewa bure kwa watoto wenye mahitaji maalum na wasio na mahitaji maalum imebuniwa kwa nia ya pekee ya kutoa elimu sambamba na viwango vya kimataifa kwa watoto wan chi hiyo ambao wanafundishwa kupitia njia rahisi ya nadharia na vitendo ambavyo vinamfanya  mtoto aweze kuelewa zaidi.

Shule hiyo ilianza mwaka 1982 ikiwa na wanafunzi nane ambapo Mama Rajapaksa alikuwa ni mmoja wa walimu wawili waliokuwepo ambao waliweza kutoa elimu kwa watoto na kutokana na jitihada zake baadhi yao baada ya kumaliza masomo wameweza kushika nyadhifa mbalimbali katika nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwakilisha Bunge la nchi.

Hadi sasa inamatawi nane yaliyopo katika mikoa mitatu ya nchi hiyo na kuwa na zaidi ya watoto 2000  huku ikiwa na malengo ya kuendeleza utu wa watoto, kutoa ujuzi wa uongozi, kuwawezesha watoto kuweza kujiamini na kujithamini, kukuza stadi za watoto, kusimamia maadili na kurejesha nidhamu kwa watoto.

Walimu wa shule hiyo hufanya kazi ya kutambua vipaji vya watoto kwani huwapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao katika matamasha ya mwisho wa mwaka na hivyo kuweza kutimiza ndoto zao na kupatikana kwa viongozi wazuri katika siku za usoni.

Wakiwa shuleni hapo wake hao wa marais na wakuu wa Serikali walijionea michezo mbalimbali iliyochezwa na watoto hao wenye umri wa chini ya miaka mitano ikiwemo ngoma, kareti na kuogelea ambayo inawajenga kiakili na kiafya na hivyo kuweza kufanya vizuri katika masomo yao. Wake hao wa Marais na wakuu wa serikali akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete walihudhuria mkutano wa 22 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliomalizika leo nchini humo.