‘Watoto Watukutu Wakipewa Nafasi Wanaweza Kubadilika’

Mama Salma Kikwete alipotembelea kituo cha kurekebisha tabia za watoto wa kike watukutu cha PERTAPIS kilichoko nchini Singapore.

Na Anna Nkinda – Singapore

WATOTO waliotengwa na jamii kutokana na tabia ya kutokuwa na maadili mazuri (watukutu) kama watapewa nafasi ya kupata mafunzo ya kutosha ya dini, elimu ya darasani na kuoneshwa msingi mzuri wa maisha wanaweza kubadilika na kuwa watoto wema.

Hayo yamesemwa leo na Mama Sahnim Sokaimi ambaye ni mkuu wa kituo cha kurekebisha tabia za watoto wa kike watukutu cha PERTAPIS kilichoko nchini Singapore wakati akiongea na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipotembelea kituo hicho.

Alisema kuwa chuo hicho kinawapokea watoto wa kike kuanzia umri wa miaka 12 hadi 21 ambao mahakama imewakuta na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uvutaji wa sigara chini ya miaka 18, utumiaji wa madawa ya kulevya na kufanya biashara ya kuuza mwili (sexual activities).

“Tuliamua kuanzisha kituo hiki baada ya kuona kuwa kuna tatizo kubwa la kuharibikiwa kwa watoto ikiwa ni pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya lakini baada ya watoto hawa kuwapa misingi mizuri ya malezi na maisha wameweza kubadilika na kuwa wasichana wema wanaofuata dini”, alisema Mama Sokaimi.

Aliendelea kusema kuwa wasichana hao wamehukumiwa na mahakama kifungo cha miezi sita hadi miaka mitatu kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya na wakiwa katika kituo hicho wanapata mafunzo ambapo baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya makosa yao wanakuwa wamebadilika kitabia na kurudi kulelewa na familia zao.

Alimalizia kwa kusema kuwa wazazi wanatakiwa kuchangia gharama za watoto wao kupata mafunzo kituoni hapo kiasi cha dola za Singapore 250 lakini wazazi wengi hawafanyi hivyo jambo ambalo linasababisha kituo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na hivyo kuomba msaada kutoka kwa wadau mbalimbali.

Kwa upande wake mama Kikwete aliwapongeza wafanyakazi wa kituo hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kurekebisha tabia za watoto wa kike ambazo hazikubaliki na jamii na kuwafanya kuwa wasichana na wamama wazuri ambao wanafanya kazi mbalimbali za kujitegemea kimaisha.

Mama Kikwete alisema kuwa jukumu la kuwalea na kurekebisha tabia za watoto ni la jamii nzima na kuwaomba wafanyakazi wa kituo hicho kuja nchini ili nao wajifunze na kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia watoto wenye matatizo kama hayo. Aidha mama Kikwete pia alitumia taaluma yake ya ualimu na kutumia muda mfupi aliokutana na wasichana hao na kuwafundisha somo la kiingereza kwa kuwaelekeza umoja na wingi wa baadhi ya vitu.

Kituo hicho chenye jumla ya wasichana 54 kilianzisha mwaka 1990 kinatoa mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu ya Sekondari na msingi kwa wale ambao walikatisha masomo yao, ufundi wa kujitegemea, mapishi, stadi za maisha, utengenezaji wa nywele, ushonaji wa nguo na mafunzo ya kiroho. Mama Kikwete ameambatana na mumewe rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Singapore kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.