Na Mwandishi Wetu, Morogoro
KAMPUNI ya Kibaran Resources inayojihusisha na utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uno kwenye Kijiji cha Epanko, imetoa msaada wa baiskeli 30 za walemavu kwa watoto wenye ulemavu katika kata ya Mahenge Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro. Baiskeli hizo zimeundwa maalumu kwa watoto wanaoishi vijijini.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi baiskeli hizo, Grant Pierce, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Kibaran Resources Tanzania alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya kijamii ambayo kampuni imeazimia kuifanya kulingana na msimamo wa kampuni hiyo wa kuwa karibu na jamiii inayowazunguka.
“Msaada huu ni sehemu ya azimio tuliloweka la kuwekeza katika jamii zinazotuzunguka. Watu wanaoishi na ulemavu husahaulika katika jamii na hawapati haki zote zinazostahili kwa binadamu. Haki za binadamu ni sawa kwa watu wote bila kujali ulemavu wao. Kukosa uwezo wa kujihudumia mwenyewe, huleta mateso kwa binadamu hasa watoto. Tunafurahi kuwasaidia watoto katika jamii hii kwa kuwapa uwezo wa kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine kwa urahisi na tunaamini itasaidia kuboresha maisha yao ya kila siku.”, Alisema Grant.
Naye kaimu mkuu wa wilaya ya Ulanga, Kisembo akimwakilisha, Francis Mitikama mgeni rasmi wakati wa shughuli hiyo ya kukabidhi baiskeli za walemavu kwa watoto alisema kuwa amefurahishwa na moyo wa kampuni hiyo kwa kujali jamii inayoizunguka haswa kundi hilo la walemavu katika wilaya.
“Nimefurahishwa sana na kitendo cha Kibaran Resources kujitolea katika kuwasaidia watoto hawa. Kwa niaba ya Wilaya, napenda kuushukuru uongozi pamoja na wafanyakazi wote wa Kibaran Resources kwa moyo wenu wa kujali watu walio katika mazingira magumu, ikiwemo watoto wenye ulemavu. Msaada huu utawawezesha watoto hawa kushiriki shughuli mbalimbali katika jamii pamoja na kufikia malengo yao, kama vile kwenda shule kama watoto wengine ili kujipatia elimu ambayo ni msingi wa maisha yao.”, alisema, Francis Miti.
Wakizungumza kwa niaba ya watoto wao, walezi wa watoto waliopewa baiskeli hizo wametoa shukurani kwa uongozi wa kampuni ya Kibaran Resources kwa kuwasaidia watoto wao kutimiza ndoto zao za kushiriki katika fursa zilizopo kwenye jamii sawa na watoto wengine wasio na ulemavu.
“Naishukuru sana kampuni ya Kibaran. Msaada huu tumeupokea kwa furaha kubwa kwani watoto wetu sasa watapata uhuru ambao hawa kuwa nao awali. Kwa sisi walezi, hii ni ahueni kubwa sana. Ni vigumu mara nyingine kwa watu kuelewa changamoto ya kulea mtoto mwenye ulemavu. Baiskeli kama hizi zinaondoa mzigo mkubwa sana kwetu”. Alisema Anton Nkawamba, mmoja wa walezi waliohudhuria shughuli hiyo.
Baadhi ya viti viliachwa katika hospitali ya mkoa ili kusaidia watoto wagonjwa wenye ulemavu wakati wanahudhuria hospitali hiyo kwa huduma za matibabu. Viti hivyo hutengenezwa na Shirika la nchini Australia liitwalo Wheelchairs for Kids, shirika ambalo wafanyakazi wake ni wastaafu wanaojitolea.