Watoto Nkasi Waajiriwa kwa Ujira wa Ndama kwa Mwaka

Mmoja wa watoto akirudisha nyumbani ng'ombe wanaotumiwa kwa kilimo Wilayani Nkasi.

Mmoja wa watoto akirudisha nyumbani ng’ombe wanaotumiwa kwa kilimo Wilayani Nkasi.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye.-1

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye.-1

Mifugo Wilayani Nkasi.

Mifugo Wilayani Nkasi.

Na Joachim Mushi, Nkasi

BAADHI ya watoto Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa hasa maeneo ya vijijini wamekuwa wakiajiriwa na familia za kifugaji kwa ujira wa ndama mmoja kwa mwaka mmoja.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi watoto hao wengi wao ni wa kabila la Wafipa na wamekuwa wakitumikishwa kazi ya kuchunga ng’ombe za wafugaji wa kabila la Kisukuma. Kibaya zaidi baadhi yao huamua kuacha kabisa masomo ya msingi na wengine masomo ya sekondari na kwenda kufanya kazi hiyo, ambayo mkataba wake huwa ni malipo ya ndama hufanywa kati ya familia ya mtoto na mfugaji.

Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa mbali na ukatili huo kwa watoto kutumikishwa, baadhi yao wamekuwa wakijikuta wakiangushiwa kipigo kikali kutoka kwa wamiliki wa mifugo hiyo hasa pale wanapopoteza mifungo wakiwa kazini. Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni maeneo hayo, ulibaini kuwa mtoto anayetumikishwa hutakiwa kuhamia katika familia ya mfugaji na kuanza kuchunga ng’ombe za mfugaji kila uchao na baada ya kukamilisha mwaka familia yake/wazazi wake hupewa ndama na mmiliki wa mifugo ikiwa ni kama ujira wa mtoto huyo.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Lunyala nje kidogo ya Mji wa Namanyere wilayani Nkasi alisema baadhi ya wazazi wanalazimika kuwaingiza watoto wao katika ajira hizo kutokana na ugumu wa maisha, hata hivyo alidai wapo watoto ambao ukimbia shule na kwenda kufanya kazi hizo.

Akizungumzia matukio hayo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye alikiri uwepo wa ajira hizo kwa baadhi ya vijiji jambo ambalo alisema wanapambana nalo na kuitaka jamii maeneo hayo ibadilike na kuacha ukatili huo.
“…Ni kweli hali hii ipo, zipo familia na wafugaji ambao wamekuwa na tabia hii ya kikatili ya kuajiri watoto wadogo na kuwatumikisha katika shughuli za kuchunga mifugo ya wafugaji hasa maeneo ya vijijini wilayani Nkasi, kibaya zaidi baadhi yao huacha masomo na kufanya kazi hizi,” alisema Mdenye.

Alisema Ofisi ya Ustawi wa jamii eneo hilo kwa kushirikiana na dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi Wilaya ya Nkasi limekuwa likijitahidi kuzunguka vijiji mbalimbali na kutoa elimu ili kuhakikisha vitendo hivyo vya kikatili kwa watoto vinakoma mara moja.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA.