Watoto Mapacha Walioungana Watenganishwa Nchi India

Watoto hao, Elikana Erick na Eliud Erick wakiwa wamebebwa na Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India Dk.Glory Joseph (kushoto) na mama mzazi wa watoto hao Bi. Grace Joel. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.

Watoto hao, Elikana Erick na Eliud Erick wakiwa wamebebwa na Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India Dk.Glory Joseph (kushoto) na mama mzazi wa watoto hao Bi. Grace Joel. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.

Na Aron Msigwa – MAELEZO

HATIMAYE watoto mapacha kutoka wilayani Kyela mkoani Mbeya waliokuwa wamepelekwa na Serikali kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha jana walirejea nchini wakitokea nchini India katika hospitali ya watoto ya Appolo walikokuwa wanatibiwa.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakiwa wameambatana na mama yao, Grace Joel na Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India ambaye pia alikuwa masomoni akisomea magonjwa ya Moyo kwa watoto Dk. Glory Joseph wamepokewa na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Nje wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Edward Sawe na baadhi ya wauguzi kutoka Taasisi ya Mifupa (MOI).

Mapacha hao wa kiume wakiwa wenye furaha na afya njema walichukuliwa katika gari maalum na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) ambako watakaa kwa muda mfupi na kisha kuruhusiwa kuelekea wilayani Kyela jijini Mbeya ambako ndiko walikozaliwa.

Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao akizungumza kwa furaha mara baada ya watoto wake kupatiwa matibabu ya kuwatenganisha kwa mafanikio makubwa alisema sasa maisha yake yamebadilika na ataishi kwa furaha na watoto wake.

“Najisikia furaha sana kwa hatua niliyofikia mpaka hapa watoto wangu Eliudi na Elikana sasa ni wazima naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa msaada ilionipatia,” alisema.

Kwa upande wake daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India, Dk. Glory Joseph akizungumzia matibabu ya watoto hao alisema kuwa hatua ya kuwatenganisha imekamilika na mwezi wa 8 mwaka huu watarudi tena nchini India kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi ya afya zao.

“Ni kwamba watoto hao wametenganishwa, kwa wakati huu wanaelekea MOI ambako watakaa kwa muda na baadaye wataruhusiwa kwenda kwao Mbeya kujumuika na jamaa zao,” alisema.

Aidha Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alisema watoto hao waliwasili jana jioni na ndege ya shirika la Oman baada ya kumaliza matibabu ya awamu ya kwanza.

Alisema upasuaji huo mkubwa wa kuwatenganisha watoto hao ulichukua saa 18 na kufafanua kuwa kati ya hizo, saa 13 zilitumika kutenganisha viungo vilivyoungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo, sehemu ya utumbo mpana, njia ya mkojo, kibofu cha mkojo na sehemu za uume huku saa 5 zikitumika kuunganisha sehemu zilizotenganishwa.

“Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mpaka sasa duniani upasuaji wa aina hii umefanikiwa mara tano  kutenganisha mapacha watoto wa kiume walioungana,” alisema.

Aliongeza kuwa matibabu hayo ni juhudi za Serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa kila mwananchi kila inapowezekana na kutoa wito kwa jamii kujenga utaratibu wa kuwafikisha mapema kwenye vituo vya afya wale wote wenye matatizo ya kiafya badala ya kuwafikisha pindi hali zao zinapokuwa mbaya.