Na Joachim Mushi
TANZANIA inapoteza zaidi ya watoto 928 walio chini ya umri wa miaka 5 ambao wanakufa kutokana na magonjwa ya kuhara ambayo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na idadi kubwa ya wananchi kutokuwa na vyoo na kutumia vyoo ipasavyo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2006 nchini umebaini takribani watoto 928 upoteza maisha kutokana na magonjwa ya kuhara, yanayochangiwa na uchafu wa vinyesi.
Akizungumza leo katika semina ya wanahabari iliyoandaliwa na taasisi ya WaterAid, kuwaelimisha waandishi wa habari juu ya afya ya mazingira na umuhimu wa matumizi ya vyoo, Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa taasisi hiyo, Marko Msambazi amesema endapo elimu sahihi itatolewa na wananchi kutumia vyoo ipasavyo kuna kiwango kikubwa cha watoto wanaweza kuepuka vifo vinavyotokea.
Akiwasilisha mada kwa wanahabari hao, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya vyoo duniani inayoadhimishwa rasmi leo, Msambazi alisema matumizi sahihi ya vyoo yakizingatiwa na usafi kiujumla Tanzania ingeweza kunusuru vifo kwa watoto wa chini ya miaka mitano takribani watoto 715 kati ya wale waliopoteza maisha mwaka 2006.
Aidha alisema asilimia 14 ya Watanzania hawatumii vyoo ikiwa ni sawa na idadi ya watu milioni 6.3 ambao kwa siku huzalisha kinyesi (mavi) tani 2.2 kwa siku. “Ukifuatilia kiafya kiasi hicho cha kinyesi kina vijidudu tele ambavyo vinamadhara makubwa kwa wananchi.
Hata hivyo aliongeza kuwa ofisi nyingi za umma pamoja na zile za baadhi ya mashirika na kampuni binafsi hazina vyoo vinavyokidhi haja jambo ambalo ni hatari kiafya, hivyo kuwataka wahusika kufanya mabadiliko mara moja kukabiliana na hali ya hatari inayoweza kujitokeza.
Naye Bi. Wilhemina Malima kutoka UNICEF akiwasilisha mada ya umuhimu wa usafi mashuleni na matumizi ya vyoo salama, alisema idadi kubwa ya wanafunzi wa kike wanaoingia hatua za utu uzima wanapoteza siku kadhaa za masomo kila mwezi, jambo ambalo linawarudisha nyuma kielimu.
“Baadhi ya wanafunzi wa kike wanashindwa kufika shuleni wanapokuwa katika siku zao…hali hii ni kutokana na shule nyingi kuwa na vyoo ambavyo havina mazingira mazuri kiafya yanayomwezesha mtoto huyu kukidhi haja zake kipindi hicho,” alisema mtaalamu huyo.
Water Aid imeamua kutoa semina hiyo kwa waandishi wa habari ili waweze kueneza elimu juu ya umuhimu wa vyoo bora, usafi na matumizi sahihi ya vyoo kwa kila mwana jamii.