MTANDAO wa Jinsia Tanzani TGNP leo umekutanisha baadhi ya watendaji wa Serikali kutoka idara za mahakama, maofisa wa Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi pamoja na wanasheria kujadili changamoto ya masuala ya sheria na sera katika kesi za ukatili wa kijinsia.
Semina hiyo kwa watendaji wa Serikali pia ilijadili nafasi za watendaji wa Serikali katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ngazi ya jamii na kutoa mapendekezo ya baadae kukabiliana na changamoto hizo.
Akizungumza katika semina hiyo akiwasilisha mada, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi alisema mfumo dume umeathiri jamii hivyo matendo mengi yanayofanywa kwa wanawake na wanaume kutegemeana na mtazamo wa jinsi zao na kuwa katika upendeleo zaidi na siyo katika nafasi ya usawa katika jamii.
“…Huu ni mfumo wala si mwanamke au mwanamme, ila ni mfumo unaohodhi madaraka, maamuzi, rasilimali nk.
Wengi huhusisha na ubabe, uonevu na ukatili ambapo katika mazingira halisi ubabe unafanywa sana na wanaumme,” alisema Bi. Liundi.
Aidha alisema lipo pengo la kijinsia tofauti; kitabia, ubora au kwa kiasi ya kutendewa kati ya wanaume na wanawake, na mara nyingine wasichana na wavulana kuhusiana na fursa za rasilimali/mali/huduma mahitaji, nafasi na mahitaji ya msingi katia jamii.
“…Majukumu ya kijinsia ni mitizamo inayojengeka katika familia/jamii kuhusu shughuli/majukumu ya wanawake na wanaume ambapo shughuli/majukumu fulani yanaoneka ni ya wanawake na mengine ni ya wanaume. Mitazamo hii inajengeka na kuathiriwa na umri, mila na tamaduni, dini, mazingira na mabadiliko ya kiuchumi, na kisiasa; kukua kwa maendeleo, sera za kijamii na kiuchumi…,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya wanawake na wanaume wote wanashiriki katika shughuli za uzalishaji lakini kazi na shughuli azifanyazo mwanamke hazionyeshi matokeo yake waziwazi kama zile azifanyazo mwanaume katika jamii hali inayosababisha kupuuzwa kwa mchango wake katika jamii.
“…Mwanaume anakuwa na kazi ambazo nyingi ni rasmi kama vile uongozi na majukumu yake, na vile vile kufanya kazi zenye hadhi ya juu ukilinganisha na mwanamke anayefanya kazi nyingi za kuhudumia
Majukumu haya ni zile kazi ambazo wanajamii wanazifanya ili kuhakikisha upatikanaji na kuwepokwa vitu muhimu katika kuendeleza jamii, kwa mfano huduma za pamoja kama vile maji, huduma ya afya, elimu,” aliongeza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi (CRC) cha TAMWA, Glagness Munuo akiwasilisha mada katika semina hiyo alisema ukatili wa kijinsia ni jambo ambalo linawanyima uhuru wanaume, wanawake na watoto kufurahia haki za msingi za kibinadamu na kufanya wapendayo.
Aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia unatokana na tofauti za kijinsia na baadhi ya mila na desturi potofu ambazo husababisha kuwepo kwa tofauti za kijinsia katika ngazi mbalimbali za jamii. Aidha alibainisha kuwa ukatili wa kijinsia unaendelea kufichwa kwa sababu unaonekana kuwa ni kitendo cha siri ambacho mtu mwingine hastahili kukifahamu.
Hata hivyo kutokana na kuwepo wanaharakati na vyombo vya habari suala la ukatili wa kijinsia kuliweka bayana inaeleweka zaidi kwa watu. Aliyataja madhara ya vitendo vya ukatili kuwa ni pamoja na wahusika kujeruhiwa vibaya, ulemavu, kifo, magonjwa ya zinaa na Ukimwi Matatizo ya afya ya uzazi. Mengine ni pamoja na Mimba kuharibika kwa akinamama, Hofu, Kutokwa na damu nyingi, Mimba zisizotarajiwa.