Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kubadilika katika kuwatumikia wananchi pamoja na kutekeleza majukumu yao.
Dk. Shein aliyasema hayo alipokuwa akifunga Semina Elekezi juu ya Kuimarisha Uhusiano baina ya Viongozi wa Kisiasa na Kiutendaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huko katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa dunia imebadilika, zama zimebadilika, maisha yamebadilika na mazingira nayo yamebadilika hivyo hakuna budi na viongozi hao nao wabadilike katika dhana nzima ya kuwatumikia wananchi.
Alisema kuwa lengo na dhamira kubwa ni kubadilika hivyo kuna kila sababu kwa viongozi hao kutilia mkazo dhana hiyo ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wanaowangoza hasa walio ngazi za chini.
Dk. Shein akifunza semina hiyo ya siku tatu, aliwataka viongozi hao kujiamiani katika kutekeleza majukumu yao na kueleza matumaini yake makubwa katika kuleta maendeleo nchini.
“Sisi ni viongozi, tunawajibu wa kubadilika ili kuweza kupata mafanikio zaidi ikiwa ni pamoja na kuwatumikia wananchi’,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk Shein alitoa pongezi kwa Jumuiya ya Madola kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kuweza kusaidia semina hiyo, alitoa pongezi kwa watoa mada, washiriki pampja na sektarieti chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Naye Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd alishiriki katika semina hiyo ambapo alieleza umuhimu wa kupewa habari kwa wananchi hasa wanaoishi vijini wakiwemo wakulima.
Semina hiyo iliyojumuisha mada 12, hatimae ilikuja na maazimio mbali mbali ikiwa ni pamoja na kila taasisi yenye vyanzo vya mapato, iweke mkazo katika ukusanyaji na kuziba miaya ya uvujaji mapato. Kuongezeka kwa mapato kutapelekea serikali pamoja na mambo mengine kuongeza maslahi ya wafanyakazi.
Azimio jengine ni wananchi wanaoishiriki katika kilimo, wawezeshwe kwa kupatiwa ardhi ya kilimo itakayowawezesha kuzalisha zaidi na kwa tija. Jengine ni jitihada zichukuliwe katika kudhibiti magendo ya karafuu nchini na kuhakikisha kuwa utambulisho wa karafuu ya Zanzibar inakubalika kimataifa.
Mipango Miji isimamiwe na itekelezwe ipasavyo ili kukidhi ujenzi holela hasa katika maeneo ya kilimo na maeneo ya vyanzo vya maji.
Kuhusu suala zima la rushwa, semina hiyo ilikujan na azimio la Sheria ya kuzuia Rushwa Zanzibar ipitishwe kwa lengo la kupambana na wanaotoa na wanaopokea rushwa kwa mujibu wa sheria. Pia, wafanyakazi wafanye tathmini utendaji wao kazini na kupitia utaratibu huo wafanyakazi wawe wanazawadiwa utendaji bora na isisubiriwe Mei Mosi.
Katika semina hiyo pia, wajumbe walipata nafasi ya kutoa michango yao kutokana na mada mbali mbali zilizowasilishwa ambapo walionesha nia na adhma ya kutekeleza kauli mbiu na dhima ya semina hiyo ambayo ni kubadilika.
Akitoa mada juu ya Majukumu na Wajibu wa Wakuu wa Idara na Taasisi mbali mbali za Serikali na Umuhimu wa Maadili katika uendeshaji wa serikali, Dk. Abdulhamid Mzee alisema kuwa viongozi wote walioteuliwa lazima watambue kuwa wamepewa heshima kubwa na wanapaswa kuiheshimu na kuithamini.
Alisema kuwa wakati wote wanakiwa kazini na nje ya kazi wanatakiwa kuwa mfano mzuri wa tabia njema kwa wanaowaongoza na wananchi kwa jumla hivyo haitarajiwi kiongozi kuwa na tabia isoyofaa katika jamii.
Semina hiyo hiyo ni muendelezo wa semina ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo mwanzo ilianyika kwa viongozi wa kisiasa wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Watedaji Wakuu Serikalini wakiwemo Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Maafisa Tawala wa Mikoa na Wilaya. Kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘WATENDAJI LAZIMA TUBADILIKE’