Wateja wa Vodacom kupata taarifa za afya na kimapenzi

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imezindua huduma ya ‘Young Africa Live’ itakayowawezesha wateja wake kupata taarifa sahihi za afya, mahusiano na ngono kuanzia Desemba Mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kampuni hiyo inaeleza kupitia huduma hiyo wateja wa Vodacom watapata fursa ya kuunganishwa na wadau wa masuala ya afya na mahusiano ya jinsia ikiwa ni pamoja na kujibiwa maswali watakayokuwa wakiuliza kwa simu zao.

‘Young Africa Live’ ni huduma itakayowaunganisha wanajamii kitaarifa kupitia simu za mkononi na kutoa burudani na fursa ya mazungumzo na kubadilishana taarifa na uzoefu katika mada za mapenzi, ngono, mahusiano, jinsia na afya ya uzazi.

“Tunaimani kwamba huduma hii itasaidia jamii hususan vijana ambapo kupitia taarifa za kiafya wataweza kuwa na mahusiano yenye tija na kujikinga na maambuzkizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Rene Meza.

“Kila juhudi ni muhimu katika vita ya kupunguza athari za virusi vya Ukimwi na Ukimwi, matatizo ya afya ya uzazi katika jamii ikiwemo vifo. Taarifa sahihi ni nyenzo muhimu katika mapambano haya, hivyo huduma hii ni wazi itapunguza pengo la ukosaji wa habari muhimu za afya kwa wanajamii,” ameongeza Rene.

Akizungumzia taratibu alisema ili mteja wa Vodacom aweze kunufaika na huduma hii ya kwanza nchini kutoka Vodacom anapaswa kuwa na huduma ya Intaneti kwenye simu yake na kupitia Portal ya Young Africa Live ataunganishwa na wanajamii wengine na wadau wa afya kwa urahisi. Huduma hii ni ya bila malipo kwa wateja wa Vodacom wa malipo ya baada.

“Tunategemea vijana wengi kutumia fursa hii kujifunza, kubadilishana mawazo na uzoefu juu ya masuala ya afya na mahusiano na hatimae kuwa chachu ya mabadiliko ya tabia,” alisema Rene.

Huduma ya Young Africa Live imefanya vizuri nchini Afrika Kusini na kuwa tegemeo la chanzo cha habari kwa vijana ambao kupitia mazungumzo ya pamoja yamesaidia kubadili mitazamo ya vijana katika mapenzi, ngono na masuala ya afya ya uzazi.