BENKI ya NMB imeingia makubaliano na kampuni ya Shirika la ndege ya Fastjet ambapo kwa sasa wateja wake wanauwezo wa kukata tiketi na kufanya malipo kupitia benki ya NMB. Ushirikiano huo unawawezesha wateja wa Benki ya NMB na wasio wateja wa benki hiyo kulipia tiketi zao kupitia mtandao wa kibenki.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo juzi jijini Dar es Salaam Meneja Mkuu wa Fastjet, John Corse alisema kuingia makubaliano hayo kunarahisisha huduma za upatikanaji wa tiketi pamoja na kuongeza huduma zao katika maeneo ambayo hawana ofisi.
Alisema Benki ya NMB inamtandao mpana na matawi zaidi ya 170 nchi nzima hivyo huduma hiyo ya tiketi kwa mtandao wa benki utasaidia zaidi kwa wateja wao. “…Wateja sasa watakuwa na uwezo wa kupata huduma za tiketi kupitia mtandao wa benki ya NMB na matawi yote ya Benki ya NMB kitendo ambacho kinaendeleza kutimiza ahadi ya kurahisisha huduma siku zote kwa wateja wao,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker alisema kuingia kwa makubaliano hayo kihuduma kunaendelea kusogeza huduma kwa wateja wao kwa kutumia simu za mkononi. “…Tunajivunia kitendo cha wateja wetu kuendelea kutuunga mkono kwa upande wetu sisi tunawahakikishia tutaendelea kutoa huduma bora na nafuu na kulingana na mahitaji yenu,” alisema Bi. Bussemaker.
Alisema huduma hiyo itawezesha wateja wa NMB Mobile zaidi ya milioni moja waliojisajili katika huduma hiyo kununua tiketi zao na kufanya malipo ya tiketi za ndege ya Fastjet moja kwa moja kupitia simu zao na matawi ya benki ya NMB.