‘Watanzania Watakiwa Kuwajali Yatima’

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Montage Tanzania, Teddy Mapunda

Na Anna Nkinda – Maelezo

WATANZANIA wametakiwa kujenga tabia ya kuwajali watu wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ili nao wajione kana kwamba wana wazazi ingawa baadhi yao wamefiwa na wazazi wao.
 
Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Montage Tanzania, Teddy Mapunda wakati wa sherehe za sikukuu ya Eid Mubarak zilizofanyika katika Shule ya Sekondari ya watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ya WAMA-Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
 
Mapunda alisema ingawa watoto hao hawana wazazi lakini kama jamii itawajali na kuwaonesha upendo hawatahisi tofauti ya kutokuwepo kwa wazazi wao kwani kutakuwa na watu wanaowajali kama vile wazazi wao wako hai.
 
Mkurugenzi huyo pia aliipongeza shule hiyo kwa kuzisaidia shule za jirani za Sekondari za Mahege na Nyamisati ingawa nao wanapata msaada kutoka kwa wafadhili kwa kuimarisha miundombinu ikiwa ni pamoja na kujenga majengo, kutoa vitabu, kuweka umeme wa jua na kuwapatia walimu wa mazoezi ambao wakimaliza vipindi vya kufundisha katika shule ya WAMA-Nakayama wanaenda kufundisha katika shule hizo.
 
Naye Kaimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Suma Mensah alisema kuwa shule yake inawanafunzi 322 wa kidato cha kwanza hadi cha nne kutoka mikoa yote ya Tanzania ambao ni watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
 
Kwa upande wa michezo alisema kuwa wanashiriki michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu kwa wanawake na mpira wa mikono kwa wanawake, drama na riadha. Aliongeza kuwa eneo la viwanja wanalo kubwa na la kutosha lakini hawana viwanja rasmi pia wanakabiliwa na upungufu wa vifaa vya michezo kama vile jezi, viatu na mipira.
 
“Kwa mara ya kwanza shule yetu ilishiriki mashindano ya UMISETA mwaka 2012 na kufikia ngazi ya mkoa hali ambayo imetutia moyo na tunaamini kuwa ipo siku wanafunzi wetu watafika ngazi ya Taifa”, alisema Mwalimu Mensah.
 
Wafanyakazi wa kampuni ya Montage Tanzania waliamua kusherehekea sikukuu ya Eid Mubarak na wanafunzi hao ili kuonyesha kuwa wanawajali na kuwathamini. Pia waliwapatia zawadi za jezi nne za michezo mbili za mpira wa miguu na mbili za mpira wa mikono na mipira 10, mitano ya mpira wa miguu na mitano ya mpira wa mikono.