Watanzania watakiwa kumgeukia Mungu

Mchungaji Deborah Malassy wa Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches (TFC)

WATANZANIA wametakiwa kuacha kulalamika na badala yake wamgeukie Mungu na kuiombea nchi kama ambavyo neno la Mungu limeagiza. Wito huo umetolewa Machi 8, 2012 katika ibada maalum ya kuliombea Taifa la Tanzania iliyofanyika katika ukumbi wa Sinza Christian Centre jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Maombi hayo yaliandaliwa maalum ili kuliombea Taifa, kuziombea ndoa na familia ili Mungu aweze kuzidisha ulinzi wake.

Akizungumza na wanawake wa madhehebu mbalimbali walioshiriki maombi hayo, Mchungaji Deborah Malassy wa kanisa la Tanzania Fellowship of Churches (TFC), alisema wakati umefika wa Watanzania kumlilia Mungu na kuliombea Taifa badala ya kuendelea kulalamikia kila jambo linapotokea.

“Akinamama sisi ni jeshi kubwa, huu si wakati wa kulalamika, bali tunapaswa kuingia magotini na kumlilia Mungu. Mbele ya wanawake kuna utetezi, kuna vibali na ushawishi, mbele ya wanawake kuna machozi ambayo Mungu hawezi kuyaacha yapotee bure,” alisema.

Mchungaji Deborah alisema maombi kama hayo yanabadilisha historia ya nchi au ya mtu binafsi na kama watu watamgeukia Mungu, Taifa litapona kama ambavyo Mungu aliahidi kwenye neno lake kupitia Mambo ya Nyakati wa Pili sura ya 7 mstari wa 14.

Mchungaji Deborah aliongoza maombi ya kuliombea Taifa, akamuombea Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu pamoja na Baraza zima la Mawaziri ili waweze kupata suluhisho la matatizo yanayoikabili nchi ikiwemo mgomo wa madaktari.

Naye Mama Mchungaji Tina Mdobilu wa kanisa la TAG Manzese ambaye aliombea kuhusu vyama vya siasa, alisema maombi ni sawa na reli na kwamba reli inapoishia na treni ndipo inapoishia. Alisema kushindwa kuomba ni dhambi na mtu anaposindwa kuomba anazuia mapenzi ya Mungu.

Aliwaasa akinamama hao kuacha kuwa na maombi ya kibiriti bali wawe na maombi ya kila mara na kubwa wapende kuombea amani ya Taifa la Tanzania. “Tuviombee vyama vya siasa ili vijae watu wanaoijua kweli, wanaoguswa na kujali shida za wananchi,” alisema.

Aliwaonya akinamama hao wasitumbukie kwenye kundi la watu wanaoibukia sasa hivi ambao kazi yao kuwasema vibaya viongozi kwani kufanya hivyo ni kutafuta laana.

“Katika agano la kale imeandikwa kwamba mtu haruhusiwi kumsema vibaya kiongozi wa nchi kwa sababu kiongozi anaweza kuruhusu Baraka au laana katika nchi,” alisema na kutoa mifano ya Sauli na Daudi.

Naye Mchungaji Elizabeth Nsajigwa aliombea kuhusu imani ambayo haina mashaka na kusisitiza kuwa hata kama mtu atafunga na kuomba vipi, kama hana imani, maombi yake ni bure. “Tunatakiwa tuwe na imani itendayo kazi,” alisema.

Mchungaji Elizabeth alitumia fursa hiyo kuwaombea Watanzania ambao wanajishughulisha na kazi za kilimo, ufugaji na biashara ili mashamba na mifugo yao vizae sana na wao pia wapate soko la uhakika na bei nzuri.

Maombi hayo yaliongozwa na Mama Askofu Aikael Shega, Mama Mchungaji Tina Mdobilo, Mchungaji Ency Mwalukasa, Mwl. Glory Samwel, Mchungaji Elizabeth Nsajigwa na Mchungaji Deborah Malassy ambaye ndiye muandaaji wa maombi hayo ya kitaifa.

Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches (TFC) ndilo huandaa Mkesha Mkubwa wa Kitaifa ambao hufanyika Desemba 31 ya kila mwaka ili kuliombea Taifa la Tanzania.