Watanzania wamechoka kuomboleza

 

 

 

Taifa bado linaomboleza jamaa na ndugu waliokufa katika ajali mbaya ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa likiendelea kujengwa katika mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es Salaam, kauli na maoni mbalimbali yamekuwa yakitolewa hasa ikitiliwa maana kwamba watu 34 wamethibitika kufa katika janga hilo kubwa zaidi kupata kutokea katika historia yakuporomoka kwa majengo marefu nchini.

Katika janga hilo lililotokea siku ya Ijumaa Kuu wiki iliyopita, watu 18 walijeruhiwa baadhi wamepata matibabu hospitalini na kuruhusiwa huku wanane wakiendelea na huduma hiyo, hata hivyo ingawa kazi ya kusaka waliokufa imekwisha kuhitimishwa,

kuna vichwa viwili vya binadamu ambavyo vinasubiri uthibitisho wa kidaktari kujua kama nao walikuwa sehemu ya walioangukiwa na jengo hilo au la. Kwa maana hiyo vifo vinaweza kuongezeka hadi kufikia watu 36. Idadi hii ni kubwa kwa vigezo vyovyote vile, lakini hata kama ingelikuwa chini ya hapo hizi ni roho za watu zimetolewa kwa sababu kuu moja, UZEMBE.

Tunajua tangu wiki iliyopita zimeandikwa tahariri nyingi juu ya janga hili, nasi tunaheshimu na kutambua fika kwamba ujumbe unaweza kuwa umewafikia wahusika wote wanaobebeshwa lawama kutokana na janga hili, pamoja na hayo tungependa kuwa wazi kuwa hakuna idadi ya tahariri zitakazoandikwa kutosheleza kufikisha ujumbe kwa wahusika kwa sababu taifa hili linataka kulazimishwa kuzoea vitu viwili; mosi, kutokujali, na mbili kutokuwajibika.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2006 baada tu ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani mambo matatu yalikuwa ni changamoto kubwa na nzito yaliyohitaji kujituma kwa dhati kwa watawala ili ama kuyashinda au kuzembea na kukubalia kuwa mateka wa majanga hayo.

Haya ni tatizo sugu la mgawo wa umeme ambao ulikuwa ukielezwa kutokana na ukame uliosababisha mabwawa ya kuzalisha umeme kukosamaji; tatizo kubwa la ujambazi wa kutumia silaha uliokuwa umetingisha taifa kila mahali kuanzia mitaani kwenye maduka ya watu binafsi hadi ndani ya mabenki na kuibwa kwa fedha nyingi mara nyingi wahalifu wakitoroka bila kukamatwa; lakini pia kulikuwa na tatizo kubwa lililojitokeza la kujenga majengo makubwa ya ghorofa kienyeji mno. Yote haya yaliundiwa mkakati.

Leo itoshe tu kujielekeza kwanye suala la ujenzi wa ovyo kama siyo holela. Kwamba ilitokea ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kuua mtu mmoja, na pia kulikuwa na kiburi cha fedha cha watu kutokutii vibali halali vya ujenzi wa majengo marefu na kujiamulia kuongeza idadi ya ghorofa kwa kadri walivyotaka wao, ni mambo ambayo serikali ya awamu ya nne ilianza kukumbana nayo.

Kwa bahati nzuri, maamuzi yalifanyika kwamba kila mmoja ni lazima aheshimu sheria, kanuni na taratibu zote za ujenzi kwa mujibu wa mipango miji na mahitaji halisi ya eneo na eneo.

Ni katika kuamua kuchukua hatua kwa serikali ndiko kulishuhudiwa kwa baadhi ya maghorofa yakibomolewa kwa kukataa tu kufuata sheria, kanuni na taratibu nyingine za mipango miji, lakini pia Watanzania walishuhudia kuundwa kwa kamati ya ukaguzi wa majengo ambayo ilipewa kazi kubwa ya kukagua majengo yote ya maghorofa mjini na kujiridhisha kama kweli yalikuwa yanakidhi vigezo vyote vya usalama.

Kamati ile ilifanya kazi kutokea Ofisi ya Waziri Mkuu, ilitembelea na kukagua baadhi ya majengo, lakini kwa hakika ilikoishia na ripoti yake ilikuwa na nguvu gani ya kuzuia majanga ya kuporomoka kwa majengo marefu kama ilivyotokea wiki iliyopita, ni vigumu kusema kuwa umma una taarifa yake kamili.

Leo tunaomboleza kama watu wasiokuwa na kumbukumbu, tunaonyesha kila aina ya hisia kwa janga hili, lakini ukweli ni kwamba hata kama tukiomboleza vipi hatuwezi kuwarejesha wenzetu 34 ambao maisha yao yamekatishwa kilatili mno katika ajali hii; hatuwezi kabisa kuwafariji wafiwa wote kwa sababu maneno matupu yatawafufua wapendwa wao, lakini pia nguvu kazi hii ya taifa iliyopotea haiwezi kurejea asilani!

Ni kweli kuna mwamko mkubwa wa kunega majengo marefu ya kisasa katika miji yetu kwa sasa; ni jambo jema na zuri kwa maendeleo ya miji na hata wakazi wake, majengo haya yanaongeza shughuli za kiuchumi na kijamii, yanachangia ukuaji wa uchumi kwa sababu fedha nyingi zinatumika katika shughuli ya ujenzi. Ni jambo zuri na halali kabisa.

Hata hivyo, uzuri wa kukua kwa sekta ya ujenzi unachafuliwa na watu wa aina mbili, mosi wakandarasi wenye tamaa ya kuwa na majengo makubwa bila gharama kwa maana ya kuchakachua viwango vya ujenzi kama mali ghafi zinazofaa na vipimo vyake, na kundi la pili ni wasimamizi, kuanzia kwenye halmashauri hadi kwenye wizara husika.

Kote kumejaa ulafi na tamaa mbaya ya kupokea kitu kidogo ili kufumbia macho vigezo vya kitaalam vinavyokubalika katika ujenzi.

Kibaya zaidi, haya yanatokea wakati ilikwisha kuundwa kamati ya kukagua majengo na kumaliza kazi yake, kwa bahati mbaya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyokuwa na wajibu wa kusimamia kazi hii, ipo na inaendelea kuwako, lakini majengo yanaporomoka bila yenyewe kuwa na majibu ya majanga haya. Tunasema wazi Watanzania wamechoka kulia na kuomboleza, ni wakati sasa wa viongozi kuwajibika, haitatosha tu kukimbizana na vidagaa katika kadhia hii, safari hii wananchi wanataka kuona papa akivuliwa!

CHANZO: NIPASHE