Watanzania Waitikisa Marekani kwa Utapeli

Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula.

Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula.

BAADHI ya Watanzania wanaoishi Marekani huenda wakaozea jela baada ya kutiwa hatiani na wengine kukiri mahakamani kuhusika katika utapeli na wizi wa mamilioni ya Dola za Marekani, kupitia mikopo na upangishaji wa nyumba.

Hukumu ya hivi karibuni ni ya Mtanzania, Mokorya Cosmas Wambura (41) ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela na faini zaidi ya Dola 400,000 (zaidi ya Sh660 milioni) baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kutumia vitambulisho vya wizi na taarifa za kibenki za kughushi kufanya udanganyifu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Maryland, Deborah Chasanow katika hukumu yake, pia alisema Wambura ataendelea kuwa chini ya uangalizi kwa miaka mitano baada ya kumaliza kutumikia kifungo jela.

Wambura ambaye ni mkazi wa Takoma Park, Maryland alitiwa hatiani kwa kula njama za wizi wa mtandao na kuhusika katika matukio mawili tofauti ya kujipatia fedha kwa udanganyifu, akitumia vitambulisho vya wizi.

Hukumu dhidi ya Wambura imetolewa wakati ambao Watanzania wengine kadhaa wakiwamo wawili waliokuwa washirika wake wakisubiri hukumu zao, baada ya kukiri kufanya makosa ya utapeli, kujipatia fedha kwa udanganyifu na wizi wa kutumia mtandao.

Watanzania hao ni Edgar Tibakweitira, ambaye pia anajulikana kwa majina mengine; Edgar Julian, Charles Edgar Tibakweitira na Edgar Gaudious Tibakweitira ambaye licha ya kukiri makosa yake pia alikubali kutoa gari lake aina ya Range Rover, kama sehemu ya malipo ya fedha atakazoamriwa kulipa na mahakama.

Baada ya kukiri makosa yake, hukumu ya Tibakweitira itatolewa Novemba 3 mwaka huu Saa 04:00 asubuhi, na kwa mujibu wa sheria za Maryland, adhabu ya makosa yake ni kifungo kisichozidi miaka 30 jela na faini ya Dola za Marekani milioni moja (Sh1.66 bilioni).

Mbali na Tibakweitira ambaye ni mkazi wa Severn, Maryland, Mtanzania mwingine ambaye pia alikuwa mshirika wa Wambura ni Mrisho Mavuruma Mzese ambaye alitiwa hatiani Mei 1, 2014 kwa makosa 11 yanayohusiana na utapeli na wizi kwa njia ya mtandao.

Hukumu dhidi ya Mzese imepangwa kutolewa Agosti 7 mwaka huu Saa 8:00 mchana, huku akikabiliwa na adhabu kama ya Tibakweitira kwa mujibu wa sheria za Maryland.

Aprili 22 mwaka huu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Jimbo la Maryland ilitoa taarifa kuhusu Watanzania wengine wawili ambao walikiri mahakamani makosa ya kujipatia fedha kwa udanganyifu baada ya kutoa taarifa za uongo kuhusu ununuzi wa nyumba na ukarabati wa nyumba hizo.

Watanzania hao ni mkazi wa Ashburn, Virginia, Nsane Phanuel Ligate (42) ambaye ni wakala wa uuzaji wa nyumba na mshirika wake wa karibu Cane Mwihava (43) mkazi wa Bowie, Maryland.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na kulipa faini ya Dola za Marekani milioni moja (Sh1.66 bilioni), watakapohukumiwa na Jaji Chasanow. Hukumu dhidi ya Mwihava imepangwa kutolewa Oktoba 14 mwaka huu saa 7:00 mchana wakati Ligate amepangwa kuhukumiwa siku mbili baadaye, Oktoba 16, 2014 saa 4:00 asubuhi.

Mtanzania mwingine ambaye anasubiri hukumu ni Gladyness Silaa (35) mkazi wa Bowie, Maryland ambaye pia alikiri kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mashtaka mapya
Siku tatu kabla ya hukumu ya Juni 16 mwaka huu, Wambura alijikuta katika sakata lingine pale alipokamatwa na polisi na watu wengine watano, wakihusishwa na utapeli mwingine wa kujipatia Dola za Marekani 3.5 milioni (karibu Sh5.8 bilioni) kupitia mikopo ya fedha kwa ajili ya nyumba.

Taarifa ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Jimbo la Maryland inawataja watuhumiwa wengine katika kesi hiyo mpya kuwa ni Tibakweitira na mkewe Flavia Makundi (41), Mkazi wa Gambrills, Maryland, Carmen Johnson (46), Mwihava na Annika Boas (36) ambaye anaishi Mount Ranier, Maryland.

Katika kesi hiyo mpya, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia vitambulisho vya wizi, nyaraka za ajira za kughushi na taarifa za uongo za mikopo kujipatia kiasi hicho cha fedha kupitia biashara za nyumba.

Wanashtakiwa kwa makosa 21 ambayo wanadaiwa kuyafanya kati ya Machi 2007 na Novemba 2008 kwa kujipatia fedha za ziada katika biashara za nyumba kadhaa kinyume cha thamani halisi ya nyumba hizo katika soko.

Tibakweitira ambaye alikuwa wakala wa biashara ya nyumba akiongoza kampuni za Century 21 Advantage Realty na Elite Real Estate Group, anatuhumiwa kuongeza ‘cha juu’ kwenye mauzo ya nyumba, akiambatanisha vielelezo vya kughushi vinavyoonyesha kwamba nyumba husika zilikuwa zimefanyiwa ukarabati, kumbe siyo kweli. Kwa kufanya hivyo, mtuhumiwa huyo alijipatia kiasi kikubwa cha fedha za mkopo kutoka benki.

Maelezo ya mashtaka yanasema watuhumiwa hao sita walitumia vitambulisho feki na vya wizi, fomu feki za mikopo, nyaraka za kibenki zilizoghushiwa na taarifa za uongo za mikopo kushawishi wakuu wa taasisi za utoaji za fedha na nyumba kutoa mikopo kwa Wambura, Mwihava na Boas ambao pia walikuwa wanunuzi feki wa nyumba.

Taarifa za kiuchunguzi zinadai kuwa, fedha hizo ambazo zilipatikana kwa njia ya udaganyifu ziliondolewa kwenye akaunti za waliodaiwa kuwa wakopaji na kuhamishiwa kwenye Kampuni za Destiny Property Management na Destiny Property Management Co. — shell ambazo ni mali ya Tibakweitira kwa malengo kwamba zilipaswa kutumika kwa ajili ya ukarabati.

Hata hivyo, ukarabati huo haukuwahi kufanyika, badala yake fedha zilizoombwa kama mkopo kwa ajili hiyo ziligawanywa kwa watuhumiwa wote sita. Kwa mujibu wa hatia ya mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kusababisha hasara ya Dola za Marekani milioni moja (zaidi ya Sh1.66 bilioni) kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Nyumba,ambayo ndiyo inayodhamini mikopo.

Pia hasara hiyo inazigusa taasisi nyingine zikiwamo Shirika la Taifa la Mikopo ya Nyumba na Shirika la Taifa la Makazi, taasisi ambazo zilinunua nyumba husika baadaye gharama zake kuonekana kuwa kubwa kuliko uhalisia.

Watanzania hao ni sehemu ya mamia ya watuhumiwa ambao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani baada ya kuundwa kwa kikosikazi cha kukabiliana na uhalifu katika sekta ya nyumba eneo la Maryland, chenye uwakilishi wa taasisi zote zinazohusika na sekta hiyo na vyombo vya dola.

Baadhi ya Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Washington DC walikiri kufahamu uwepo wa kesi dhidi ya Watanzania hao na kwamba hilo ni jambo la kawaida kwa wahalifu kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Sheria zipo kwa ajili ya wahalifu, sasa kama ikitokea mtu akafanya uhalifu, wenzetu hapa wako makini sana, lazima utakamatwa na kufikishwa mahakamani na ukitiwa hatiani unafungwa au unatozwa faini kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Lily Munanka ambaye ni Mkuu wa Utawala katika ubalozi huo.
CHANZO: Mwananchi