*Umoja wa Watanzania Ujerumani Wapata Viongozi Wapya
MKUTANO Mkuu wa Watanzania waishio nchini Ujerumani uliofanyika Septemba 29, 2012 mjini Frankfurt katika Kitongoji cha Raunheim umefanikiwa kupata viongozi wapya watakao iongoza Jumuiya hiyo. Miongoni mwa malengo ya mkutano huo pamoja na maazimio mengine ilikuwa kufanya uchaguzi wa viongozi wapya wa umoja huo, jambo ambalo lilifanikiwa.
Awali akizungumza mgeni rasmi katika mkutano huo Naibu Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Ali Siwa aliwapongeza Watanzania kwa kufanikiwa kuunda Umoja wa Watanzania nchini Ujerumani (UTU), ambao kwa sasa ndio mwamvuli mkuu wa mshikamano wa Watanzania wote Ujeruman.
Aidha alisema Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani ipo wazi wakati wowote iwapo umoja huo utahitaji ushauri wowote ikiwa ni juhudi za kuleta maendeleo ya umoja na Watanzania kwa ujumla. Hata hivyo aliwataka Watanzania nchini humo kuwa na mshikamano kwani, ushirikiano huo ndiyo utakaokuwa ufunguo na sauti ya maendeleo yao na vizazi vya Watanzania waishio ugenini na pia wa nchini Tanzania.
Baada ya nasaha hizo wanachama kwa utaratibu walifanya uchaguzi kupata viongozi wapya watakao kiongoza chama hicho, ambapo nafasi ya Mwenyekiti ilichukuliwa na Mfundo Peter Mfundo, huku Makamo wake akiwa ni George Mtalemwa. Nafasi ya Katibu ilikwenda kwa Bi. Tulalumba Mloge, huku upande wa mtunza fedha (Mweka Hazina) ukinyakuliwa na Bi Mwamvua Dugala Merkel.
Umoja huo wa Watanzania Ujerumani (UTU) ndio chombo pekee kilichopata usajili kwenye serikali ya ujerumani, na kutambuliwa kisheria, ambacho kinawaunganisha watanzania wote wanaoishi ujerumani, na ndio Daraja linalowaunganisha watanzania waliopo Nyumbani na kwengineko ughaibuni. Kwa watanzania wanaopenda kujiunga na umoja wa watanzania ujerumani (UTU) milango ipo wazi, wasiliana na kamati.utu@googlemail.com