Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es Salaam
WATANZANIA waishio nchini Uingereza wametoa msaada wa vitu mbalimbali zikiwemo nguo, viatu na vifaa vya watoto kuwasaidia wakazi wa Mabwepande walioathiriwa na mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam Desemba 2011.
Akikabidhi msaada huo kwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki kwa niaba ya watanzania hao Mkurugenzi wa kampuni ya Usafirishaji wa Mizigo ya Serengeti (Serengeti Freight Fowarders Ltd), Chris Lukosi amesema hatua ya watanzania hao waishio nchini Uingereza imefikiwa baada ya kuguswa na matatizo ya mafuriko yaliyowakumba wakazi wa jiji la Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana.
Amesema wao kama kampuni ya kusafirisha mizigo inayofanya kazi nchini Uingereza wameungana na watanzania wengine waishio nchini humo kuhamasishana ili kuona namna ya kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo.
“Kampuni yetu inafanya kazi za kusafirisha mizigo kutoka nchini Uingereza, sisi kama kampuni ya Kitanzania kwa kushirikiana na Watanzania wengine waishio Uingereza tuliguswa sana na tatizo la mafuriko tukahimizana na kufanikiwa kupata boksi 20 ikiwa ni mchango wa vitu mbalimbali,” amesema Lukosi.
Ameeleza kuwa hali ya ukusanyaji wa michango ya vitu mbalimbali kutoka kwa watanzania hao ilianza taratibu na baadaye kupata nguvu na kuifanya kampuni hiyo kuchukua jukumu la kuisafirisha bure misaada hiyo kuja nchini Tanzania bila gharama yoyote. Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo amewapongeza watanzania hao kwa moyo wa upendo waliouonyesha kuwasaidia waathirika hao.
Amesema wakazi hao ambao sasa wanaishi Mabwepande wataona kuwa hawako peke yao na kuwa bado kuna watanzania wengi wanaendelea kuwakumbuka katika hali waliyopitia.
“Kwenu ninyi watanzania muishio Uingereza hii ni dalili nzuri kwa kukumbuka nyumbani, nawahakikishia kuwa Serikali inawaunga mkono na wakazi wa Mabwepande watahisi furaha kwa michango yenu na kuona kuwa wanathaminiwa na watanzania wenzao licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili”
Amewaomba watanzania hao na wale wanaoishi nchi nyingine kuendelea kushiriki na kuchangia masuala mbalimbali yanayotokea nchini Tanzania yakiwemo ya elimu, vitabu na madawati.