NA BASHIR NKOROMO, DOGGUAN, CHINA
WATANZANIA wanaoshi nchini China wametakiwa kushikamana na kuitangaza Tanzania kwa kuonyesha tabia njema .
Akizungumza na Wanajumuia ya Watanzania wanaoishi China, baada ya kukutana nao katika mji wa Dongguan, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, wasipokuwa na mshikamano na kuwaonyesha tabia njema wenyeji wao, Wataharibu sifa ya Tanzania Kimataifa ambayo inafahamika kwamba ni nzuri kwa miaka mingi.
Kinana ambaye hupo nchini China na ujumbe wa watu 14 kwa ajili ya ziara ya mafunzo katika nyanja mbalimbali, alikutana na Watanzania hao, baada ya kuamua kumtembelea katika hoteli ya Exhibition International hoteli, jana, Machi 12, 2013, ili kumsalimia na kubalishana naye mawazo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Watanzania hao walisema, wamekuwa wakiishi nchini China kwa mahusiano mazuri kutokana na maadili waliyolelewa nayo ya Kitanzania, lakini hali hiyo huenda ikaingia dosari kutokana na kuwepo Watanzania ‘feki’ ambao wamekuwa wakiingia China kwa pasi za Tanzania na kufanya maovu.
“Hawa Watanazania bandia wakiishaingia hapa hujitambulisha kuwa ni Watanzania, hata wakiulizwa pasipoti ya Tanzania wanayo, lakini cha ajabu ukiwauliza wanakotoka Tanzania wanababaika na hata lugha ya Kiswahili hawajui sawasawa. Utamkuta mtu anajua kusalimia tu, anasema ‘mambo’ basi, sasa jamani kuna Mtanzania ambaye hawezi kuzungumza kiswahili, lakini akawa na uwezo wa kuja ugenini kama huku?” alisema Katibu wa Jumuia wa Watanzania hao waishio China, David Chgamla.
Alisema, kutokana na hali hiyo, Wachina sasa wameanza kupunguza imani yao kwa Watanzania kiasi kwamba mtu anapojitambulisha kuwa ni mtanzania wakati akiihitaji huduma anatazamwa mara mbili mbili kuthibitisha uaminifu wake.
Akizungumzia baadhi ya Watanyabiashara kutapeliwa au kuziwa bidhaa zisizo na ubora au kwa bei isiyo halali, Katibu huyo alisema, wengi wanakutana na mikasa hiyo kwa sababu wanakifika China wanakwenda mahali ambapo siyo sahihi kwa mahitaji yao na hivyo kutahamaki wakiingia hasara.
“Lakini Ndugu Kinana, Jumuia hii tuliyounda hivi karibuni na kuwa na uongozi huu mpya, nina imani itawasaaidia Watanzania wengi kutopoteza fedha au mali zao wanapokuwa wamekuja hapa kibiashara, kwa sababu tunajipanga vema kuhakikisha kila atakayekuwa anakuja akipenda anakutana na sisi kwa ajili ya msaada”, alisema.
Uongozi wa Wanajumuia hiyo ya Watanzania unaundwa na John Luhumbiza (Mwenyekiti), Abraham Merishani (Makamu Mwenyekiti), David Chamla (Katibu Mkuu) na Msaidizi wake ni Aboubakari Mwinyi.