Na Mwandishi Wetu
WATEJA walioko kote nchini sasa wana fursa ya kupata taarifa sahihi zinazohusu ubora wa huduma na bidhaa mbalimbali zilizo sokoni kwa njia rahisi ya mitandao ya kijamii pasipo na malipo yoyote.
Huduma iliyozinduliwa jana baada ya utafiti wa muda mrefu imepewa jina la Sokoni Tanzania ambapo watumiaji wa mtandao wa Facebook wataipata kwa kupitia www.facebook.com/sokonitanzania na watumiaji wa mtadao wa Twitter wataipata kwa kufullow akaunti ya @sokonitanzania.
Huduma inatoa fursa wateja kote nchini waliokwisha kununua au kutumia bidhaa na huduma mbalimbali kutoa “Grades” kutoa tathimini zao katika bidhaa na huduma walizonunua katika masoko kote nchini kwa mtindo wa grades. Grade A inawakilisha bidhaa au huduma yenye viwango vya hali ya juu sana ambayo inabeba maksi 5 . Grade B inawakilisha bidhaa au huduma yenye viwango vya hali juu. Grade C inawakilisha bidhaa au huduma zenye viwango vyenye hali kati zinazohitaji maboresho. Grade D na E inawakilisha bidhaa au huduma hafifu zilizoko sokoni. Majumuisho ya tathimini za wateja yatatolewa kila siku kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii nchini.
Huduma hii itawasaidia wateja ambao wamekuwa wakipata changamoto ya kupata taarifa za uhakika kuhusu ubora wa huduma zilizoko katika sehemu mbalimbali nchini. Vilevile huduma hii inatoa fursa kwa wamiliki na watafiti wa bidhaa kufahamu ubora halisi wa bidhaa na huduma zao na hivyo kuwapa nafasi ya kuziboresha na kulifanya soko la Tanzania kuwa na huduma na bidhaa bora.