WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi; Mh. Mwigulu Nchemba (Mb) ametembelea Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambapo alikutana na Menejimenti ya NIDA na kupokea taarifa ya maendeleo ya shughuli ya Usajili na Utambuzi wa Watu.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa Vitambulisho vya Taifa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA; Ndugu Andrew Wilson Massawe, amemweleza Mh. Waziri mpaka sasa NIDA imekamilisha awamu ya kwanza ya usajili wa Watumishi wa Umma, ambapo watumishi 500,605 wamesajiliwa nchi nzima. Na NIDA sasa inaendelea na hatua ya mwisho kukamilisha uhakiki wa watumishi hao ili kutoa namba za utambulisho na kuunganisha Kanzi Data ya NIDA na Utumishi, ambapo watumishi watakuwa wakitambuliwa kwa alama za zao za vidole.
Mbali na kukamilisha Usajili wa Watumishi; NIDA imepanga kuanza kutoa namba za Utambulisho wa Taifa kwa wananchi wote nchi nzima waliosajili kwenye daftrati la NEC. Namba hizo zitawawezesha kuanza kunufaika na utambulisho wa Taifa kwa kupata baadhi ya huduma toka kwa wadau mbalimbali wakati wakiendelea na taratibu za kukamilisha usajili wao ili kupata vitambulisho vya Taifa.
Kwa sasa NIDA ina taasisi na mashirika 35 ambayo yameanza kutumia Kanzi Data (Database) kuhakiki wateja wanaofika kupata huduma zikiwemo taasisi za fedha; huku Taasisi na kampuni nyingine 70 zimeonyesha nia ya kutumia mfumo huo kuhakiki taarifa za wateja wanaowapa huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Mwigulu amesema hii ni fursa ya pekee kwa wananchi kuhakikisha wanapata nambari za utambulisho wa Taifa itakayowawezesha kuanza kunufaika na fursa mbalimbali zinazokosekana kwa sasa kutokana na Taifa kutokuwa na Vitambulisho vya Taifa. Amesema hatua hii nzuri na kubwa kwa Taifa, kwani katika muda mfupi asilimia kubwa ya watanzania watakuwa wameingizwa kwenye Kanzi Data (Database) ya NIDA na hivyo Serikali kuanza kutimiza ile ndoto ya miaka mingi ya Taifa kuwa na Kitambulisho cha Taifa.
“..Nia ya Serikali ni kuona kila mtu anatambulika na kupitia mfumo huu wa Utambuzi na Usajili kuwapunguzia watanzania mzigo wa kubeba kadi lukuki za utambulisho. Kwa kuwa mfumo huu ni wa kielektroniki una uwezo wa kufanya mambo mengi, hata kutumika kufanya malipo katika maduka makubwa na huduma nyingine muhimu na hivyo kurahisisha maisha ya kila mtanzania” alisisitiza
NIDA imepanga kuanza kutoa namba za utambulisho (National Identification Number – NIN) kwa wananchi wote waliosajiliwa katika daftari la Mpiga kura, zoezi ambalo limepangwa kuanza mwezi Desemba mwaka huu. Mbinu mbalimbali zitatumika kuhakikisha kila mtanzania aliyesajiliwa NEC anapata namba yake pale alipo; pamoja na kutoa utaratibu wa namna ya kukamilisha usajili wake ili kupata utambulisho kamili. Zoezi hili halitahusisha wananchi ambao tayari wana Vitambulisho vya Taifa.
Aidha; Waziri Mwigulu amewaasa watanzania kuwa wazalendo linapofika suala la kuweka pingamizi kwa wale watu ambao siyo raia kwani lazima kabla ya kutoa kitambulisho lazima kila mwombaji kuhakikiwa na kuthibitishwa uraia wake kabla ya kupewa kitambulisho.
Hii ni ziara ya kwanza kwa Waziri Mwigulu kutembelea NIDA tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; ambapo mbali na kutembelea makao makuu ya NIDA na kufanya mazungumzo na Menejimenti pia alipata fursa ya kutembelea kituo cha uhifadhi na uchakataji Taarifa (Data Centre) na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na NIDA.