Watakiwa kuwasaidia wanafunzi walemavu

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba Maendeleo na Makazi, Goodluck Ole Medeye ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo wa Arumeru Magharibi, akizungumza na mmoja wa wanafunzi wenye ulamavu Costantine Sulley katika shule ya vipaji maalum, Iliboru ya mkoani Arusha mara baada ya kukabidhi msaada wa baiskeli kwa wanfunzi wenye ulemavu shuleni hapo jana, msaada uliogharimu zaidi ya milioni 4.9 kushoto ni diwani wa Kata ya Moivo Sarubare Lendisa. Picha na Janeth Mushi.

Na Janeth Mushi, Arumeru

WADAU nchini kwa kushirikiana na jamii wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwasaidia wanafunzi walio na walemavu wa viungo na kuhakikisha kuwa wanapata elimu kama haki yao kimsingi.

Rai hiyo ilitolewa leo na Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba Maendeleo na
Makazi, Goodluck Ole Medeye wakati alipokuwa akikabidhi msaada wa viti kwa wanafunzi wenye ulemavu, katika Shule ya Sekondari ya Vipaji maalum ya Iliboru, wilayani hapa Mkoa wa Arusha.

Naibu huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, alisema kuwa iwapo jamii itajitokeza kuwajali kwa kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu, wataweza kuwasaidia waweze kujiendeleza kielimu.

“Wananchi tuwasaidie, tuwathamini wanafunzi wenye ulemavu kwani
ulemavu wa viungo siyo ulemavu wa akili na ndiyo maana wako katika
shule hii ya vipaji maalum,”

“Tuwasaidie na kuwajali kwa kuhakikisha wanapata elimu katika
mazingira rafiki, ili waweze kuchagia maendeleo katika taifa kwani nao wana uwezo wa kujitegemea iwapo tutawaunga mkono, bila kusahau kuwa ulemavu hauombwi wala kununuliwa bali unakuja tu,” alisisitiza Ole Medeye.

Akikabidhi misaada hiyo Naibu huyo alisema kuwa ameamua kutimiza ahadi aliyotoa shuleni hapo mwaka jana wakati alipokwenda shuleni hapo katika mahafali na kuona wanafunzi wenye ulemavu wakiwa katika
mazingira magumu.

“Nilisikitishwa sana wakati wa mahafali mwaka jana bada ya kuona mmoja wa wanafunzi ambaye ni mlemavu wa viungo, akitembea kwa mikono, ndiyo maaa nimetekeleza ahadi niliyoweka kuwasaidia baiskeli hizi,” alisema

Aidha aliwataka wazazi katika maeneo mbalimbali nchini wenye watoto
wenye ulemavu wa viungo kutowaficha watoto wao na badala yake
wawapeleke shule ili wapate elimu ambayo ni haki yao kimsingi.

Wakati huo huo aliwataka wanafunzi kutojihusisha na mambo ya siasa na badala yake wazingatie masomo yao huku akiwaasa walimu shuleni hapo kutokueneza siasa shuleni.

Baiskeli hizo zina thamani ya zaidi ya sh. milioni 4.9 huku katika shule ya Sekondari ya Eluai iliyopo kata ya Nduruma akikabidhi viti 50 na meza 50 kwa ajili ya wanafunzi shuleni hapo ambazo zinagharimu zaidi ya shilingi milioni 4.5.

Aliwataka wabunifu wa majengo ya shule kuhakikisha wanapojenga majengo hayo kubuni majengo yatakayo kuwa rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu

Baada ya kupokea misaada hiyo mmoja wa wanafunzi shuleni hapo mwenye ulemavu, Costantine Sulley alimshukuru kiongozi huyo, na kudai kuwa baiskeli hiyo itamsaidia kwenda mahali popote itakayomuongezea ufanisi katika elimu.

Ofisa Elimu Sekondari katika halmashauri ya Arusha, Sebastian Sesoro
aliiomba serikali kutatua changamoto ya nyumba za walimu, kutokana na walimu wengi wanaopangiwa shule za vijijini kukimbia kutokana na
kutokuwa na nyumba za walimu.