Na Mwandishi Wetu
JAMII ya Kitanzania, imeaswa kuwaangalia kwa jicho la huruma watu wasiojiweza na wenye mahitaji maalum ili kuwaweza kuishi vizuri na kujiona kuwa ni sehemu ya jamii pamoja na mapungufu waliyokuwa nayo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi misaada mbalimbali kwa kituo cha kulelea watoto ya tima na wanoishi katika mazingira magumu cha Friends of Don Bosco iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa bodi ya Benki ya KCB, Dk. Edmund Mndolwa alisema makundi maalumu yanahitaji upendo na msaada wa wana jamii ili waweze kuishi vizuri.
Dk. Mndolwa alisema kuwa, Benki ya KCB inatambua umuhimu wa kuyasaidia makundi hayo na ndiyo maana kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii ime kuwa ikiyapatia misaada mbalimbali ya kijamii.
“Leo Benki ya KCB imetoa msaada wa vifaa mbalimbali na vyakula vyenye thamani ya shilingi milioni nne na nusu. Msaada huu siyo mkubwa sana lakini ni wazi kuwa utawasaidia watoto wanaolelewa katika kituo hiki. Makampuni mengine na watu binafsi wanapaswa kutambua kuwa hata kidogo walichonacho wakikitoa kinaweza kuleta tofauti,” alisema
Mwenyekiti huyo alisema kuwa msaada utitolewa na Benki ya KCB ni muendelezo misaada mbalimbali ambayo Benki hiyo inaitoa mwaka hadi mwaka na kuongeza kuwa kwa kipindi hiki cha Octoba hadi Desemba benki ya KCB imetenga shilingi milioni 180 kwa ajili ya kuisaidia jamii.
Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi wa kituo hicho Theobald Triphone alisema kuwa msaada uliotolewa na benki ya KCB umekuja wakati muafaka kutokana na kuwa kituo kinakabiliwa na matatizo mengi.
“Msaada huu kwetu ni mkubwa sana. Kituo kinakabiliwa na matatizo mengi na kibaya zaidi hatuna mfadhili wa kudumu jambo ambalo ni tatizo kubwa.
Watoto hawa ambao baadhi ni yatima na wengine waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu wahitaji chakula,malazi, mavazi na elimu, tunawaomba wana jamii waiige benki ya KCB kwa kuwasaidia,” alisema
Baadhi ya vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda, magodoro, vyandarua, mashuka, madaftari, kalamu, unga, maharage, mchele sukari pamoja na mafuta ya kupikia.