Beatrice Lyimo – MAELEZO
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kutoa maoni na mapendekezo ili yatumike kuboresha Rasimu ya Sera mpya ya Maendeleo ya Utamaduni ya mwaka 2016 itakayochukua nafasi ya Sera ya Maendeleo ya Utamaduni ya mwaka 1997.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Lugha wa Idara ya Utamaduni wa wizara hiyo Bi. Hajjat Shani Kitongo wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu kuifanyia mabadiliko Sera ya mwaka 1997 ili iweze kukidhi mahitaji na mabadiliko ya kijamii.
Amesema maoni yatakayotolewa na wananchi yatajikita katika maeneo yanayothamini na kuenzi Maadili, Mila na Desturi, kuendeleza matumizi Sanifu na Fasaha ya Lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa, kuwa na tafiti endelevu za Lugha za Asili kwa ajili ya kuzihifadhi na kuongeza misamiati ya Lugha ya Kiswahili.
Ameongeza kuwa maboresho hayo yanalenga kuwa na bidhaa na miundombini endelevu katika Tasnia ya Filamu na michezo ya kuigiza yenye viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa vinavyozingatia Mila, Desturi na maadili ya Taifa, pamoja na kuwa na uwekezaji endelevu na mfumo jumuishi wa utaratibu wa kazi katika sekta ya utamaduni.
Bi. Kitongo amefafanua kuwa wananchi watatuma maoni yao kupitia barua pepe au kuleta maoni yao kwa mkono moja kwa moja Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo au kutuma maoni kupitia barua pepe, christopher.mhongole@habari.go.tz pia kupitia tovuti ya wizara ya www.habari.go.tz.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo Mwanzala Kayoka amesema kuwa lengo la kufanya mabadiliko hayo ni kuboresha Sera hiyo kulingana na wakati haswa katika matumizi salama na sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Sekta ya Utamaduni.
“Lengo ya kuleta mabadiliko katika Sera hii si kuunda Sera mpya bali ni kuiboresha kulingana na wakati na kuongenza yale yaliyopungua haswa katika mfumo wa TEHAMA hivyo hupelekea kuleta mfumo sahihi wa kuratibu masuala ya Utamaduni nchini” Ameongeza Mkurugenzi huyo.
Amesema kuwa ukusanyaji wa Maoni hayo umeanza Machi 4, 2016 hadi Machi, 25 Mwaka huu, na kuwaomba wadau na wananchi wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni yatakayosaidia uboreshaji wa Sera ya Maendeleo ya Utamaduni ya mwaka 2016.