Watakiwa Kusimamia Malezi na Maadili ya Watoto

Watoto

Na Anna Nkinda – Maelezo, Sumbawanga

WANANCHI wametakiwa kusimamia malezi na maadili ya watoto wao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu juu ya makuzi, hata kama mila zinazuia kufanya hivyo wawatafute wazee ili waweze kuongea na vijana.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), wakati akizungumza na Umoja wa Wanawake wa Mkoa wa Rukwa (Rukwa Women in Action – RUWA) katika ukumbi wa mikutano Manispaa ya Sumbawanga.

Mama Kikwete ambaye yuko mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu alisema kuwa mama ni muhimili mkubwa wa familia yeye ndiye anayemlea baba na watoto, hata kama baba atatoa pesa za kutunzia familia lakini bado muangalizi mkuu wa familia ni mama.

“Wahimizeni mabinti wasome shule hata kama ninyi hamjasoma naamini mnaelewa umuhimu wa shule, simamieni elimu ya watoto wenu ili waweze kusoma kwa bidii na mkijidhatiti ipasavyo watasoma hadi kufikia ngazi ya chuo kikuu.

Katika suala la elimu mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto nyingi zaidi ukilinganisha na wa kiume wakanyeni watoto wenu kwani shule nyingi ni za mchanganyiko washirikiane na watoto wa kiume katika masomo tu na siyo mambo mengine kwani binti akipata ujauzito au maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) ndoto zake za maisha kwa kipindi kile inapotea. Ni mabinti wachache walioweza kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwasisitiza wanawake hao kujitokeza kwa wingi kuomba na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pindi zinapotangazwa katika mkoa huo na waungane kwa pamoja kumpigania mwanamke mwenzao pale atakapogombea kwani mwanamke ni kiongozi mzuri ndani ya familia na jamii pia.

Mama Kikwete alisisitiza, “Kuna baadhi ya wanaume wanawakataza wake zao kugombea nafasi za uongozi hii si sawa na hawawatendei haki ya msingi kwani katiba ya nchi inasema kuwa kila mtu anahaki ya kuchagua na kuchaguliwa na wanawake wengi waliopewa nafasi ya kuongoza wameweza”.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Manyanya alisema kuwa manispaa ya Sumbawanga pekee inawatoto yatima 536 ambao wengi wao wamepotelewa na mama zao na watoto 17 hawana wazazi wote wawili hivyo basi kina mama wa kikundi hicho wanakazi kubwa ya kuwalea watoto hao.

Injinia Manyanya alisema, “Tunaishukuru Taasisi ya WAMA kwa kuendelea kuwachagua na kuwasomesha watoto yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi kwa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo toka mwaka 2010 hadi 2013 vijana wa kike 12 kutoka mkoa huu wamesomeshwa”.

Akisoma taarifa ya umoja huo Leonora Jairos ambaye ni mwanachama alisema kuwa malengo waliyonayo ni kuwahamasisha na kuwaelimisha wanawake juu ya umuhimu wa elimu hasa ya mtoto wa kike, kuelimisha jamii juu ya afya za uzazi wa mpango salama,kutoa elimu kwa kina mama juu ya maisha halisi ili kujinasua kutoka hali tegemezi na kuongeza jitihada za kupunguza maambulizi ya VVU.

“Hadi sasa tumefanikiwa kuwaunganisha wanawake wapatao 200 ambao ni wakulima, wajasiriamali na wafanyakazi katika manispaa ya Sumbawanga, tumewatembelea watoto yatima na kuwachangia vitu mbalimbali kwa mahitaji yao ya kila siku, kufanya tamasha na kuwahamasisha wanawake kushiriki katika michezo na mazoezi ili kuboresha afya zao”, alisema Jairos.

Alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mwamko wa wananchi katika suala la elimu hasa la kuwasomesha watoto wa kike, mila kandamizi kwa wanawake zilizopo katika mkoa huo na uwezo mdogo wa umoja wa kuweza kuwafikia wasichana mashuleni ili kuwapa maadili juu ya umuhimu wa elimu.

Umoja huo ulianzishwa Septemba 22, 2012 kwa wazo la Mkuu wa mkoa huo Injinia Manyanya ambaye aliona kuna umuhimu wa kuwaunganisha wanawake wote ili waweze kujiinua kiuchumi, kujitambua na kujiendeleza kielimu na kiafya na kubadilisha mtazamo wao ili kila mmoja aweze kupiga hatua mbele ya kimaendeleo na kuwaamsha walio chini zaidi hasa wale wa vijijini.