Maisha 2012 hayashikiki-Watabiri

MCHUMI MKUU WA BENKI YA STANDARD CHARTER, GERARD LYION

IMETABIRIWA kuwa mwaka 2012 utakuwa mwaka mwengine mbaya kiuchumi kwa bara la Ulaya, ingawa ahuweni ya kiuchumi katika masoko yanayoinukia na Marekani huenda ikaufanya uchumi wa dunia kutokupoteza muelekeo moja kwa moja.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Reuters, hakuna sababu za kuufurahikia mwaka wa 2012. Mataifa mengi makubwa duniani yanaelekea kwenye mtikisiko wa kiuchumi, masoko ya hisa yanaonekana yataweza kurudisha sehemu tu ya hasara iliyopata katika mwaka wa 2011 na wawekezaji hawana uhakika wa wapi pa kuwekeza mitaji yao.

Nchi nyingi zenye uchumi mkubwa katika zile zinazotambuliwa kama masoko yanayoinukia, kama Brazil na China, zinapaswa kujikaza zaidi kwa mwaka ujao. Zote zilijikuta zikikabiliwa na kudhoofika kwa kasi ya uchumi miezi ya hivi karibuni, kutokana na kukazwa kwa sera za kifedha na kupanda kwa gharama za maisha.

Mchumi mkuu katika benki ya Standard Chartered, Gerard Lyons, anasema kwamba uchumi wa dunia bado unakuwa, ingawa ni hadithi ya dunia mbili tafauti. Ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2012, bara la Ulaya litaudidimiza uchumi wa dunia, katika nusu ya pili ya mwisho, China itauinua uchumi huo.

Kuna pia vitisho vyengine kwa uchumi wa dunia kwa mwaka ujao, vikiwemo kwa mabadiliko ya serikali kupitia uchaguzi kwenye mataifa makubwa kiuchumi duniani na pia kuendelea kwa “saratani” ya mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, wachumi wengine wana matumaini kwamba deni la nje la eneo linalotumia sarafu ya euro halitapindukia mipaka na kusababisha mgogoro mwengine wa kifedha wa kilimwengu, kwa sababu wameona dalili za ukuwaji kwa mataifa yanayosafirisha bidhaa kwa wingi barani Ulaya.
Pia inaaminika kuwa uchumi wa Marekani umefanya vyema zaidi mwaka huu wa 2011 kuliko vile wengi walivyokuwa wakiudhania. Inatarajiwa kwa mwaka 2012, uchumi wa taifa hilo kubwa kabisa duniani utakuwa kwa asilimia 2.2, ikilinganishwa na asilimia sifuri kwenye eneo la sarafu ya euro.
“Jambo kubwa lisilofahamika barani Ulaya na Marekani ni kuwa makampuni makubwa, yaliyoweza kwueka hisabu zake sawa, yana uwezo wa kuwekeza makwao yakitaka. Na hilo linaweza zaidi kutokea Marekani kuliko Ulaya.” Anasema Lyons.

Licha ya viongozi wa Ulaya kuchukuwa hatua ya kihistoria kuelekea umoja madhubuti zaidi wa kifedha mwishoni mwa Disemba 2011, wachumi walionya tangu mwanzo kwamba hilo halitauzuia mgogoro wa madeni kuingia mwaka wake wa tatu na kuchukuwa nafasi ya vichwa vya habari.
Matokeo ya Reuters yanaonesha wasiwasi kwamba viongozi hawafanyi ya kutosha kuiinua uchumi, ikipigwa mifano ya Hispania na Italia ambako kunatarajiwa kuwa na miezi kadhaa ya machungu ya mtikisiko wa uchumi. Kwa sasa, eneo zima la sarafu ya euro liko kwenye mtikisiko na litakuwa hivyo hadi, kwa uchache, katikati ya mwaka ujao.
Mchumi Juan Perez-Campanero wa Santander, anasema kwamba kanda ya sarafu ya euro inaendelea kuwa chanzo cha ukosefu wa utulivu wa kiuchumi na kifedha kwa dunia nzima.

Juu ya ikiwa Hispania na Italia nazo zitakuja kuhitaji msaada wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya hapo mwakani, wachumi walioulizwa na Reuters hawakuweka wazi, lakini 27 kati ya 56 wamesema hapana.

Katika uchunguzi wa mwezi Novemba uliowashirikisha wachumi na watunga sera 20 wakubwa duniani, umeonesha kuwa 14 kati yao hawaamini ikiwa mataifa ya kanda ya euro yataweza kujikwamua kutoka hali yake ya sasa. Japan inatarajiwa kuinuka kidogo kwa asilimia 1.8 hadi kufikia mwezi Aprili mwakani, lakini itakuwa imeponea chupuchupu na kutumbukia kwenye mgogoro wa madeni.

-DW