Rajab Mkasaba, Hanoi, Vietnam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametembelea Taasisi ya Utafiti wa Ufugaji wa Samaki mjini Hanoi, Vietnam na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iko tayari kupeleka ujumbe maalum wa watalamu nchini humo ili waende kujifunza kwani utaalamu huo unaweza kuisaidia Zanzibar kiuchumi.
Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo inatokana na azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukuza mashirikiano na uhusiano na Vietnam hasa kwa kuanzisha ziara za kimafunzo kwa viongozi na wataalamu wa pande zote mbili hasa ikizingatiwa kuwa tayari Vietnam ina uzoefu mkubwa juu ya sekta hiyo.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa wataalamu wote wa pande mbili hizo watakaa pamoja kwa lengo la kuandaa programu maalum zitakazosaidia sekta hiyo ya ufugaji ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu vijana ili waweze kupanua soko la ajira kwa kujiajiri wenyewe hasa kwa vile Zanzibar ni visiwa vilivyozungukwa na bahari.
Aidha, Dk. Shein aliueleza uongozi wa Chuo hicho kuwa miongoni mwa mada kuu zilizozungumzwa kati yake na Rais wa nchi Mhe. Truog Tan Sang ni pamoja na kuimarisha mashirikiano katika sekta ya kilimo na uvuvi kati ya Zanzibar na Vietnam.
Nayo uongozi wa chuo hicho ulieleza kuwa uko tayari na wazo hilo la Dk. Shein na kumueleza jinsi taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1963, ilivyopiga hatua katika tafiti zake mbali mbali juu ya ufugai wa samaki.
Akitoa maelezo kwa Rais paoja na wajumbe wengine waliohudhuria hafla hiyo fupi katika taasisi hiyo, Dk. Phan Thi Van alieleza kuwa jinsi taasisi hiyo inavyotoa elimu kuanzia ngazi za chini hadi kufikia Shahada ya Uzamifu katika fani hiyo na kuweza kupata mafanikio makubwa.
Dk. Shein pia, alitembelea Taasisi ya Sayansi ya Kilimo iliyopo nje kidogo ya mji wa Hanoi na kuweza kupata maelezo juu ya maendeleo ya Taasisi hiyo kutoka kwa Dk. Nguyen Van Bo na kueleza jinsi sekta hiyo ilivyopewa kipaumbele nchini humo.
Kwa maelezo ya uongozi wa Taasisi hiyo, uleleza kuwa zaidi ya asilimia 73 ya wananchi wa nchi hiyo wanategemea sekta ya kilimo kama ndio shughuli kuu ya maisha yao huku akisisitiza kuwa tayari wamekuwa na ushirikiano na nchi kadhaa za Afrika ikiwemo Msumbiji ambayo tayari baadhi ya vijana wake wameshaende nchini humo kujifunza.
Zao la mpunga ndio zao kubwa zaidi ambalo linalimwa katika hekta zipatazo milioni 7.3 ikifuatiwa na mazao mengine kama vile mahindi, kahawa, korosho, mpira, chai, mbogamboga, matunda, nazi, miwa na mengineyo.
Katika upande wake Dk. Shein aliueleza uongozi wa Taasisi hiyo kuwa kilimo kwa wananchi wa Zanzibar ndio uti wao wa mgongo akimaanisha kuwa ndio sekta ambayo inategemewa sana katika shughuli za wananchi katika maisha yao ya kila siku hasa kilimo cha mpunga.
Alisema kuwa licha ya matumizi ya mpunga kuwa makubwa huko Zanzibar lakini uzalishaji wake bado haujawa mkubwa na asilimia kubwa ikifkia 80 huingizwa kutoka nje ya nchi, hivyo kupanua wigo wa kimaendeleo katika kilimo hicho kwa nchi ya Vietnam kutasaidia kukuza zao hilo kwa upande wa Zanzibar.
Alieleza kuwa mbali ya juhudi hizo pia, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mikakati maalum ya kuhakikisha suala laUsalama wa Chakula linapewa kipaumbele, huku akisisitiza haja ya kuiunga mkono Zanzibar na kuweza kushirikiana katika utaalamu na uzoefu ili Zanzibar nayo iweze kuzalisha mpunga kwa wingi.
Dk Shein pia, alitembelea Chuo cha Taifa cha Ufugaji wa Wanyama kiliopo nje kidogo ya mji wa Hanoi na kupata maelezo juu ya shughuli zinazoendeshwa chuoni hapo kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Dk. Vu Chi Cuong ambapo alisifu hatua iliyofikiwa na kuahidi kuimarisha ushirikiano ili kuweza kupata utaalamu na uzoefu wa ufugaji.
Katika mazungumzo ya pamoja kati ya Dk. Shein na ujumbe wake pamoja na uongozi wa Chuo hicho, Dk. Vu Chi Cuong alieleza utayari wa uongozi wake kutoa ushirikiano na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha ziara za kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya Vietnam na Zanzibar.
Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein pia, alitembelea Hekalu liliopo mjini Hanoi Vietnam ambalo lina historia kubwa. Pia alitembelea jumba la kumbukumbu ya Baba wa Taifa hilo la Vietnam Hayati Ho Chi Minh ambalo ujenzi wake umetokana na utashi wa wananchi wa nchihiyo, Vietnam kutokana na mazuri aliyowafanyia katika uhai wake wote ikiwa ni pamoja na kusimamia uhuru na ukombozi wa Taifa hilo.
Wakati huo huo, Dk. Shein na ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein, walitembelea Chuo cha Uvuvi kiliopo katika Jimbo la Quang Ninh mjini Halong, ambalo lipo mpakani mwa nchi hiyo na China na kupata maelezo juu ya shughuli za chuo hicho kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Dk. Thang Li Van.
Dk. Van alieleza kuwa alisema kuwa chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1962 kinatoa elimu ya sayansi na teknolojia katika sekta hiyo ya uvuvi kwa ngazi zote kiwa ni pamoja na kufanya tafiti mbali mbali. Pia, Dk. Shein alitembelea mabwawa maalum ya kufugia samaki chuoni hapo.
Katika maelezo yake alisema kuwa Dk. Van alisema kuwa chuo hicho kimekuwa na mashirikiano mazuri na jamii ambapo kimeweza kuwasaidia katika kuimaisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya ufugaji wa samaki pamoja na mikopo isiyo na riba.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa hatua zilizofikiwa na chuo hicho na kueleza kuwa Zanzibar iko tayari kuchota taaluma hiyo inayotolewa chuoni hapo kwa lengo la kuwasaidia wananchi wake hasa katika maeneo ya pembezoni mwa bahari na yale ambayo tayari inaonesha bahari imeshazidiwa na shughuli za uvuvi.
Pia, Dk. Shein alitembelea kiwanda kilicho chini ya Kampuni ya bidhaa za bahari ambacho pia, husindika samaki kiliopo mjini Halong, ambacho ni cha pekee kwa upande wa Kaskazini mwa Vietnam kinachojishughulisha na shughuli hizo, Kiwanda hicho kilianzishwa miaka 30 iliyopita. Kampuni hiyo husafirisha samaki katika nchi za Ulaya, China, Japan na Marekani ya Kaskazini ambayo pia, huagiza samaki kutoka nje ya Vietnam.
Katika maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, alizitaja aina kubwa ya samaki wanaosafirishwa na kampuni hiyo wakiwemo pweza, ngisi na ngonda na kueleza kuwa Serikali imeweza kutoka mchango mkubwa w uwekaji wa miundombinu katika kiwanda hicho ambacho hivi sasa kimeshabinafsishwa kwa wawekezaji.
Viongozi alioambatana nao katika ziara hiyo nao walipata fursa ya kujifunza mambo tofauti ikiwa ni pamoja na kuuliza masuala mbali mbali juu ya shughuli za maendeleo katika maeneo yote aliyotembelea Dk. Shein katika ziara yake hiyo nchini Vietnam.